Je, utawala mpya wa Syria unaweza kujumuisha makundi yote?
19 Machi 2025Tangu yalipoanza maandamano zaidi ya muongo mmoja uliopita, ya kuipinga serikali iliyoondolewa madarakani ya Bashar al Assad, wimbo uliokuwa ukisikika katika taifa hilo la Mashariki ya Kati, ni wa kudai ujumuishwaji wa madhehebu yote ya Wasyria.
Watu wa Syria ni wamoja hiyo ndio kauli iliyokuwa ikisikika kila mahala. Lakini wakati huohuo msemo huo maarufu kwa bahati mbaya hauakisi uhalisia wa namna mambo yalivyo ndani ya taifa hilo la Syria.
Kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka, kiasi asilimia 68 ya Wasyria walikuwa ni waraabu waislamu wa madhehebu ya Sunni, asilimia 9 hadi 13 nyingine ilikuwa ni jamii ya Waalawi ambao kimsingi ni madhehebu ya Shia na kati ya asilimia 8 na 10 ilikuwa ni Wasyria wajamii ya wakurdi.
Soma: Nani anadhibiti eneo gani nchini Syria?
Halafu kuna Wadruze, Wakristo, Warmenia, jamii ya Caucasus, Waturkmenistan, Wapalestina na Yazidi. Familia ya Assad ilipokuwa madarakani walitumia migawanyiko ya kimadhehebu na kijamii iliyokuwepo miongoni mwa makundi mbali mbali kuendelea kudhibiti madaraka.
Lakini tangu ulipoondolewa utawala huo wa kidekteta Desemba mwaka jana, Umoja wa Ulaya na washirika wengine wamekuwa wakiishinikiza Syria kufanya mabadiliko ya kuzijumuisha jamii zote katika serikali mpya ili nchi hiyo iondolewe vikwazo ilivyowekewa. Wiki iliyopita Serikali ya mpito ya Syria inayoongozwa na Ahmed al Sharaa, ilichapisha nakala ya mwanzo ya katiba mpya ya muda ya nchi hiyo.Marekani yasifu makubaliano kati ya serikali ya Syria na Wakurdi
Kwenye hili wataalamu wa masuala ya katiba wameshagusia kwamba hakuna mahala kokote wanakotajwa Wasyria wa jamii za wachache. Wazawa pia wamelalamika kuhusu kukosekana kwa uwakilishwaji katika mdahalo wa kitaifa uliofanyika hivi karibuni.
Na juu ya hilo mshauri mmoja ambaye ni mtaalamu wa mambo ya uchumi, Karam Shaa amedokeza kwamba serikali ya mpito ya Syria kwa kiasi kikubwa bado inahusishwa na kundi la wanamgambo la Hayat Tahrir al Sham (HTS), kundi ambalo liliongoza harakati za kijeshi zilizomuondowa madarakani Dikteta Bashar Al Assad mwishoni mwa mwaka jana.
Na hasa ikitajwa kwamba baraza la mawaziri 21 na wateuliwa 154 wa nafasi za maafisa waandamizi waliopewa nafasi kati mwezi Desemba na Februari mwaka huu, wengi ni wanaume na Waislamu wa madhehebu ya Sunni.Jumuiya ya kimataifa yaunga mkono mpito mpya wa Syria
Lakini kwa mujibu wa mshauri huyo kwa sehemu hili linaweza kueleweka kutokana na mazingira ya uteuzi huo ulivyofanyika ingawa aliongeza kwa kusema kwamba ikiwa hali hii itaendelea kujitoketa hapana shaka, litakuwa ni tatizo.
Hata hivyo kwa Wasyria wenyewe hawaamini ikiwa mfumo wa kugawana nafasi za uongozi kimadhehebu utafanya kazi. Miongoni mwa Wasyria waliokuwa na mtazamo huo ni Alaa Sindian mwenye umri wa miaka 32, Mshia aliyeikimbia nchi yake wakati wa vita alipokuwa akitafutwa na utawala wa Assad, na ambaye amerejea Damascus hivi sasa baada ya utawala huo kuondoshwa.
Kwa mtazamo wake anasema uhalisia wa Syria ni kwamba ni nchi yenye kukaliwa na makundi ya jamii za waliowachache.Lakini wakati huohuo hangependelea kuona viti vya bunge vinagawanywa kwa mafungu kwaajili ya kutengewa jamii hizo, iwe ni washia, waalawi au jamii yoyote ile.Jamii ya kimataifa yaahidi zaidi ya dola bilioni 6 kwa ujenzi wa Syria
Ameiambia Dw kwamba serikali inapaswa kutafuta watu kwa vigezo vya uwezo wao miongoni mwa jamii hizo.Lakini pia anaamini wakati huohuo kunapaswa kuweko majukwaa mbali mbali ambayo yanaweza kutumiwa na jamii hizo kusikika na kuzipa nguvu.
Mtizamo wa kuukataa mfumo wa kutenga nafasi za kisiasa kwaajili ya madhehebu ya waliowachache inapingwa pia na mwanaharakati wa kiraia kutoka jamii ya Wadruze, Shadi al Dubisi,mwenye umri wa miaka 29.Naye pia anaamini mtu anapaswa kupewa jukumu serikalini kutokana na uwezo wake na sio madhehebu yake.
Hali inayoikabili Syria imezikabili pia Lebanon na Iraq,ambako ulipatikana ufumbuzi. Mnamo mwaka 1989 nchini Lebanon yalifikiwa makubaliano ya Taif yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na chini ya makubaliano hayo nafasi zilitengwa kwa kuzingatia madhehebu yote yaliyokuwa vitani na yote yalipaswa kuwa na uwakilishi serikalini.Mkutano wa wafadhili wa Syria wafanyika mjini Brussels
Nchini Iraq baada ya uvamizi wa Marekani mwaka 2003 na kuangushwa kwa utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein, utawala wa Marekani ukaamuwa lazima madaraka yagawanywe kati ya jamii tatu kubwa nchini Iraq, ambazo ni Shia, Sunni na Wakurdi.