Je, Marekani itaishambulia kijeshi Iran?
19 Juni 2025Hapo jana Jumatano na usiku wa kuamkia leo milipuko iliutikisa mji mkuu wa Iran, Tehran, katika mfululizo wa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Israel.
Utawala mjini Tel Aviv umerejea kusema kuwa inao udhibiti wa anga la mji wa Tehran na imekuwa inayashambulia maeneo muhimu kudhoofisha nguvu za kijeshi za Iran na mradi wake tata wa nyuklia.
Iran nayo ilijibu mapigo usiku wa kuamkia leo kwa kuvurumisha makombora kadhaa ya masafa kuelekea Israel lakini taarifa zinasema karibu yote yalidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel.
Wimbi hilo la mashambulizi la Iran limehusisha makombora machache tofauti na ilivyokuwa mnamo siku za mwanzo za makabiliano yanayoelekea kutimiza wiki nzima.
Duru kutoka mji mkuu wa Iran, Tehran zinasema hali ya wasiwasi imetanda, mitaa ikiwa mitupu, biashara zimefungwa na mawasiliano hasa ya intaneti ni dhaifu.
Iran ilisema hapo jana Jumatano imelazimika kupunguza kasi ya mtandao wa intaneti kukabiliana na kitisho kikubwa cha udukuzi wa mifumo muhimu ya usalama ikiwemo shughuli za kibenki.
Vyanzo: Trump ameidhinisha mipango ya kijeshi kuishambulia Iran
Hayo yanajiri katika wakati ulimwengu unasubiri kuona iwapo Marekani itajiunga na Israel kuishambulia Iran hasa baada ya viongozi wa Israel kumrai Rais Donald Trump kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya dola hiyo ya kiislamu.
Trump usiku wa kuamkia leo alifanya kikao cha pili na maafisa wa ngazi ya juu wa usalama kwenye ikulu ya White House.
Mashirika kadhaa ya habari yameripoti yakinukuu vyanzo vya ndani ya Marekani vikisema Trump tayari ameidhinisha mipango ya kuishambulia Iran lakini yungali anasubiri kuona iwapo Iran italegeza kamba na kukubali bila ya masharti kuusambaratisha mradi wake wa nyuklia.
Trump aliwaambia waandishi habari hapo jana kuwa Tehran "imetumbukia kwenye matatizo makubwa" na kwamba sasa viongozi wake wameomba kwenda ikulu mjini Washington kufanya mazungumzo na Marekani.
Madai hayo ya Trump yalipingwa mara moja na Ubalozi wa Kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa.
Mapema jana Jumatano, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayattolah Ali Khamenei alisema kamwe taifa lake "halitosalimu amri" na kuionya Marekani juu ya "taathira kubwa" iwapo itaamua kujiunga na Israel kuishambulia kijeshi dola hiyo ya uajemi.
"Adhabu ambayo taifa la Iran na vikosi vyake vya kijeshi vimeitoa, vinaendelea kuitoa sasa na vinapanga kuendelea kuitoa kwa adui huyu muovu ni adhabu kali ambayo imemdhoofisha adui huyo. Ukweli kwamba marafiki zake wa Kimarekani wanaingilia kati na kuanza kutoa matamko unaonesha udhaifu na kushindwa kwao (Israel)." alisema Ayatollah Khamenei.
Juhudi za kidiplomasia zachomoza, Putin asema angependa kuwa mpatanishi
Katika kile kinachoonekana kuwa juhudi kubwa za kidiplomasia zimeanza kushika kasi kwenye mzozo huo, mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi tatu za Ulaya wanapanga kukutana na mwezao wa Iran kesho Ijumaa mjini Geneva.
Mawaziri hao Johann Wadephul wa Ujerumani, Jean-Noël Barrot wa Ufaransa na David Lammy wa Uingereza watakutana na Abbas Araghchi wakiwa pamoja na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas.
Nchi hizo tatu za Ulaya zimekuwa zikiendeleza jitihada za kidiplomasia na Iran hususani kuhusu mradi wake wa nyuklia hata baada ya Marekani kujiondoa kutoka kwenye mkataba kati ya Iran na madola sita yenye nguvu ulionuwia kudhibiti mradi wake wa nyuklia.
Shughuli za nyuklia za Iran ndiyo chanzo cha mzozo uliopo sasa. Israel inaituhumu Iran kuwa inalenga kuunda silaha za maangamizi za nyuklia madai ambayo Tehran kila wakati imeyakanusha vikali.
Katika hatua nyingine, Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema jana Jumatano kuwa yuko tayari kusaidia kuzipatanisha Israel na Iran ili kumaliza mzozo uliopo.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya kimataifa, Putin amesema anaweza kufanikisha mkataba utakaoiruhusu Tehran kuendelea na mradi wake wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia huku ikitoa hakikisho kwa Israel juu ya mashaka yake ya kiusalama.