Je, ushuru wa Marekani unamaanisha nini kwa EU?
2 Juni 2025Mahakama ya Biashara ya Kimataifa ya Marekani ilitoa matumaini ya muda mfupi kwa Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa kibiashara duniani baada ya kutangaza kusitisha ushuru wa asilimia 10 uliowekwa na Rais Donald Trump kwenye bidhaa zote zinazoingia nchini humo. Uamuzi huo ulieleza kuwa Trump alivuka mipaka ya madaraka yake ya urais kwa kutumia sheria ya mwaka 1977 kuhusu mamlaka ya kiuchumi wakati wa dharura.
Hata hivyo, matumaini hayo hayakudumu. Saa chache baadaye, mahakama ya rufaa ilisitisha utekelezaji wa uamuzi huo, na hivyo kurejesha ushuru huo kwa muda. Katika muktadha huu wa mvutano wa kisheria, swali kubwa ni, ni wapi mamlaka ya mwisho kuhusu sera ya biashara inapasa kuwa, kwa rais au bunge la Marekani.
Vita vya kibiashara vya Trump vyatawala mkutano wa BRICS nchini Brazil
Umoja wa Ulaya ulitarajia kutumia uamuzi huo kama turufu ya kuimarisha nafasi yake kwenye mazungumzo yanayoendelea na Marekani. Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya Maros Sefcovic alieleza kuwa mazungumzo yanaendelea kwa kasi, akisisitiza kuwa EU imejitolea kikamilifu kutafuta suluhisho la muda mrefu.
EU sasa ina nafasi nzuri ya kujadiliana kwa nguvu mpya
Lakini wataalamu wamegawanyika. Mbunge wa Bunge la Ulaya Bernd Lange alisema EU sasa inayo nafasi nzuri ya kujadiliana kwa nguvu mpya, kwani vitisho vya Marekani kutumia ushuru kama njia ya shinikizo vimepungua. Hata hivyo, Andre Sapir, kutoka taasisi ya uchumi ya Bruegel anaona hali kuwa imezidi kuwa ya kutatanisha. Alisema kwa wafanyabiashara, jambo baya zaidi ni kukosekana kwa uhakika wa mwelekeo wa sera.
EU kuweka shinikizo la kuondoa ushuru mpya wa Trump
Katika harakati za kupunguza mvutano, Tume ya Ulaya imependekeza mpango wa kuondoa ushuru wa pande zote - katika kile unnachokiita makubaliano ya sifuri kwa sifuri. Lakini Trump bado analalamikia tofauti ya mizani ya kibiashara, akitaka EU inunue bidhaa zaidi kutoka Marekani, hususan gesi asilia. EU tayari imeanza kubadili chanzo chake cha gesi kutoka Urusi kwenda Marekani kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Lakini ikiwa mazungumzo hayatazaa matunda, EU imesisitiza kuwa iko tayari kuchukua hatua za kujibu. Wakati huo huo, wachambuzi wanatahadharisha kuwa hata kama mahakama zitabatilisha ushuru wa "Siku ya Ukombozi" ya Trump, bado anaweza kutumia mbinu nyingine kuweka ushuru tofauti.
Kwa kifupi, mvutano huu wa ushuru haujaisha, na barani Ulaya, sintofahamu bado ni kubwa.