Je, China inaweza kushinda vita vya kibiashara na Marekani?
19 Februari 2025Muda wa chini ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa muhula wa pili wa Rais wa Marekani Donald Trump, hatua za kwanza za vita vipya vya biashara kati ya Marekani na China zimeanza kuchukuliwa. Hali hii inaambatana na ushuru wa kulipizana kisasi na tishio la madhara ya kiuchumi kwa pande zote mbili.
Baada ya Marekani kuweka ushuru wa jumla wa 10% kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka China mapema Februari, China ilijibu kwa kutangaza ushuru wa 10%-15% kwa bidhaa za Marekani kama mafuta ghafi, gesi asilia iliyolegezwa, mashine za kilimo, na bidhaa nyinginezo.
Ushuru huo wa kulipizana kisasi wa China ulianza kutekelezwa siku ya Jumatatu, siku hiyohiyo ambapo ushuru tofauti wa 25% wa Marekani kwa chuma na alumini ulianza kutumika.
Mbali na ushuru wa kisasi, China pia imetangaza udhibiti mpya wa mauzo ya nje ya madini muhimu kwa utengenezaji wa bidhaa za teknolojia ya hali ya juu kama vile semiconductors.
Beijing pia imeanzisha uchunguzi wa kisheria wa ushindani dhidi ya Google na kuiweka kampuni ya Marekani PVH Group – inayomiliki chapa za Calvin Klein na Tommy Hilfiger – pamoja na kampuni ya baioteknolojia Illumina, kwenye orodha yake ya "taasisi zisizoaminika." China pia imetoa malalamiko katika Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuhusu ushuru wa 10% uliowekwa na Marekani.
Vita vya ushuru vya Marekani na China vinarudia historia?
Wang Guochen, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Chung-Hua nchini Taiwan, aliliambia DW kwamba "hadithi ya miaka sita iliyopita inaanza kujirudia." Trump alianzisha duru ya kwanza ya ushuru kwa bidhaa za China mnamo 2018, na Beijing ikajibu vivyo hivyo, hali iliyosababisha mzunguko wa ongezeko la ushuru.
Takwimu kutoka Taasisi ya Peterson ya Uchumi wa Kimataifa (PIIE) zinaonyesha kuwa wastani wa ushuru wa Marekani kwa bidhaa za China umekuwa juu ya 19% tangu Juni 2020, wakati makubaliano ya "awamu ya kwanza" kati ya Washington na Beijing yalipositisha kuongezeka zaidi kwa ushuru.
Soma pia: Trump asema Wamarekani wataumia katika vita vya biashara na Canada, China na Mexico
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa "vita vya biashara na ushuru havina mshindi na vinaathiri maslahi ya watu wa China na Marekani."
"Tunaitaka Marekani kurekebisha makosa yake na kuacha kuingiza siasa na kuifanya biashara kuwa silaha ya mgogoro," aliongeza.
Je, ushuru wa Marekani dhidi ya China utaweza kuwa na madhara kinyume?
Haijulikani ni vigezo gani ambavyo Ikulu ya Marekani imeweka ili kupunguza ushuru mpya kwa bidhaa za China, ambao ulitangazwa kwa kisingizio cha kushindwa kwa Beijing kudhibiti usafirishaji wa fentanyl kwenda Marekani.
Hata hivyo, ushuru huo wa 10% ni tofauti kubwa na ushuru wa 60% dhidi ya bidhaa za China uliokuwa ukitajwa na Trump wakati wa kampeni yake ya uchaguzi.
Takwimu kutoka Goldman Sachs, zilizoripotiwa na The Washington Post, zinaonyesha kuwa ushuru wa China unahusu bidhaa za thamani ya dola bilioni 14 kutoka Marekani, huku ushuru wa Marekani kwa bidhaa za China ukihusisha bidhaa za thamani ya dola bilioni 525.
Nick Marro, mchumi mkuu wa Asia na mtaalamu wa biashara ya kimataifa katika Economist Intelligence Unit (EIU), aliiambia DW kuwa kwa njia nyingi, Marekani inaonekana kuwa katika nafasi ya kupata hasara zaidi katika awamu ya kwanza ya ongezeko la ushuru.
"Ushuru ni kodi inayolipwa na walaji wa Marekani," alisema Marro, akiongeza kuwa hatua hizi zimetekelezwa "bila mpangilio mzuri na bila onyo la kutosha."
Wafanyabiashara wa Marekani hulazimika kulipa bei kubwa kwa bidhaa wanazoagiza, na gharama hiyo huwapitishia walaji.
Katika vita vya kwanza vya biashara vya Trump na China, Beijing iliweka ushuru kwa bidhaa za kilimo kutoka Marekani, hususan soya, hali iliyowaathiri sana wakulima wa Marekani.
Mnamo 2023, Marekani iliagiza bidhaa za thamani ya dola bilioni 427 kutoka China, kulingana na takwimu za hivi karibuni za Ofisi ya Sensa ya Marekani. Bidhaa zilizoongoza ni simu janja, kompyuta, na vifaa vya kielektroniki vya watumiaji.
Tishio la Trump la kuweka ushuru wa 25% kwa bidhaa kutoka Canada na Mexico, ingawa liliahirishwa, limezua wasiwasi mkubwa kuhusu mtazamo wake wa biashara usiotabirika.
"Hili linazua maswali kuhusu uaminifu na uwazi, na linawatia wasiwasi sio tu washirika wa biashara wa Marekani bali pia washirika wake wa kimataifa," alisema Marro.
"Aidha, kuna hatari ya kwamba hali hii inaweza kuharakisha kuhama kutoka kwenye mfumo wa biashara wa kimataifa unaoongozwa na Marekani kwenda kwenye mfumo mbadala, pengine unaopendekezwa na China," aliongeza.
Udhaifu wa kiuchumi wa China
Mvutano mpya wa biashara unakuja wakati China inapambana na ukuaji hafifu wa Pato la Taifa (GDP) na kushuka kwa mahitaji ya ndani, kunakosababishwa na kuyumba kwa soko la mali isiyohamishika.
Ikilinganishwa na vita vya kwanza vya biashara wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, mataifa mengi yameanza kutafuta njia mbadala za ugavi na biashara ili kupunguza utegemezi wao kwa China.
Ingawa nchi zilizoendelea zinaweza kuwa makini na mashaka zaidi kuhusu kufanya biashara na Marekani chini ya Trump, "hii haimaanishi kwamba zitakumbatia China," alisema mtafiti Wang.
Aliendelea kueleza kuwa China inaweza kuelekeza mkakati wake wa biashara kwa nchi zinazoendelea, lakini uwezo wake mkubwa wa uzalishaji wa bidhaa unaweza kuwa kikwazo kwa mpango huo.
Soma pia: Jimbo la 51 la Marekani? Jinsi Canada inavyoweza kumkabili Donald Trump
Ingawa China haiko juu katika orodha ya wauzaji wa chuma na alumini kwa Marekani kutokana na vikwazo vya biashara vilivyokuwepo awali, ushuru mpya wa 25% wa Marekani unakuja wakati China inapojaribu kuuza chuma zaidi katika masoko ya kimataifa kutokana na uzalishaji kupita kiasi ndani ya nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, nchi zinazoendelea kama Mexico, Indonesia, na Thailand pia zimeanza kuwa na mashaka kuhusu uagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka China na zimeweka sera za kuzuia bidhaa zilizoagizwa kwa bei ya chini.
"Kwa kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa China inategemea mauzo ya nje, hali hii itaathiri uwekezaji wa ndani, ajira, na matumizi ya wananchi," alisema Wang.
Chaguo jingine kwa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ni kutegemea soko lake la ndani, lakini matumizi ya walaji nchini China bado yako chini.
Katika msimu wa vuli wa 2024, serikali ya China ilipitisha hatua kadhaa za kiuchumi ili kuchochea matumizi ya walaji, ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya riba na kutoa msaada wa kifedha wa dola trilioni 1.4 kwa serikali za mitaa zilizo na madeni makubwa.
Hata hivyo, kadri bidhaa nyingi zinavyoendelea kuingizwa kwenye soko la ndani badala ya kusafirishwa nje, hali hii inaweza kuongeza shinikizo kwa mahitaji ya walaji.
Soma pia: Je, EU inaanzisha vita vya biashara na China
Wananchi wa China wanaweza kufurahia bei za chini mwanzoni, lakini kuna hatari ya kushuka kwa thamani ya bidhaa (deflation).
"Pamoja na sera za kuhimiza kampuni zinazolenga mauzo ya nje kuelekeza bidhaa kwa soko la ndani, hii imepelekea kushuka kwa bei za bidhaa ndani ya China," alisema Wang.
Zaidi ya hayo, bei za chini zinamaanisha faida ndogo kwa kampuni.
"Hali hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa ukosefu wa ajira," aliongeza, jambo ambalo linaweza kuleta mzunguko mbaya unaozidi kudhoofisha matumizi ya ndani.