Je, CCM kuahirisha mkutano wake ni ishara ya mzozo?
21 Julai 2025CCM iliahirisha mkutano wake huo hadi Julai 28, mkutano ambao ulitarajiwa kuwachagua makada wa chama hicho walioonyesha nia na kuchukua fomu wakiomba ridhaa ya chama hicho, kupata ridhaa ya kukiwakilisha chama hicho katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Uamuzi wa ghafla wa kuahirisha kikao cha kamati kuu ya CCM, Jumamosi Julai 19, umezua maswali lukuki miongoni mwa wadau wa siasa Tanzania, ambao wamehoji je, ni mpasuko ndani ya chama au mkakati wa kujiimarisha zaidi ili kupata wagombea walio sahihi?
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Shule ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aboubakar Kiondo amesema hatua hiyo ni atokeo ya chama kutokuwa na upinzani wa kweli nje ya chama.
"CCM ili iwe imara, waruhusu upinzani ambao ni wa kweli nje ya chama." Aliiambia DW.
Kuibuka kwa upinzani ndani ya CCM
Ahirisho la kikao cha kamati kuu ya CCM, limekuja ikiwa ni saa chache baada ya kada wa CCM, ambaye pia alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kutangaza kuachia nafasi yake ya ubalozi akikishutumu CCM kwa mchakato dhaifu wa watia nia.
Awali Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye awali aliikosoa CCM kuhusiana na matukio ya utekaji na upoteaji wa watu, naye alizungumza kwa njia ya mtandao akisimamia hoja yake ya utekaji na kusisitiza yeye bado ni mwanachama wa CCM.
Siku chache baada ya kujiachia nafasi ya ubalozi, Julai 18, Polepole alizungumza kwa njia ya mtandao na wanachi na kukosoa vikali jinsi chama tawala cha Mapinduzi, CCM, kilivyokiuka utaratibu kwa kumpitisha mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar.
Pamoja na hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makala alitaja sababu za kuahirisha kamati hiyo na kusema sababu la ahirisho hilo ni kutokana na majina ya watia nia kuwa mengi na hivyo mchakato wa kuwachambua unafanyika.
Kamati Kuu ya CCM ilitaraia kufanya kikao chake cha uteuzi wa mwisho kwa walioteuliwa kugombea nafasi mbalimbali kwa ajili ya kwenda kwenye kura za maoni.