JD Vance akutana na Narendra Modi mjini New Delhi
22 Aprili 2025Makamu wa rais wa Marekani JD Vance amekutana na waziri mkuu wa India Narendra Modi baada ya kukaribishwa mjini New Delhi Jumatatu, huku India ikipania kupata mkataba wa mapema wa biashara kuepusha athari za ushuru wa Marekani.
Afisi ya Modi imesema kumepigwa hatua muhimu katika mazungumzo huku nchi hizo mbili zikijadiliana kuhusu vipengee muhimu vya kwanza vya mkataba wa kibiashara.
India ina matumaini ya kupata nafuu katika kipindi cha siku 90 cha kusitishwa kwa ushuru mkubwa uliotangazwa na rais wa Marekani Donald Trump mwezi huu.
Ziara ya siku nne ya Vance nchini India inafanyika miezi miwili baada ya Modi kufanya mazungumzo katika ikulu ya Marekani na rais Donald Trump, wakati ambapo India iliahidi kununua mafuta na gesi zaidi ya Marekani kusawazisha ziada ya biashara na Marekani.