JD Vance aanza ziara ya siku nne nchini India
21 Aprili 2025Makamu wa rais wa Marekani JD Vance leo anaanza ziara ya siku nne nchini India. Vance anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa India Narendra Modi mjini New Delhi baadaye leo jioni.
Wizara ya mambo ya nje ya India imesema ziara hiyo inatoa fursa ya kutathmini mafanikio na hatua zilizopigwa katika mahusiano kati ya nchi hizo mbili, huku uchumi na mashirikiano ya kibiashara yakitarajiwa kupewa kipaumbele.
Mafanikio katika sera ya kigeni na usalama pia yatakuwa katika ajenda ya mazungumzo. Vance ameandamana na mke wake Usha aliyezaliwa California na wazazi wenye asili ya India, pamoja na watoto wao watatu.
Familia hiyo itaitembelea pia miji ya Jaipur na Agra kabla kurejea Washington siku ya Alhamisi.
Vance anaitembelea India baada ya kufanya ziara mjini Roma, Italia na katika makao makuu ya kanisa Katoliki duniani, Vatican, ambako alikutana na kiongozi mkuu wa kanisa hilo, Papa Francis.