Japan, Australia kuimarisha uhusiano wa ulinzi
5 Septemba 2025Japan inaimarisha ushirikiano na washirika wa Marekani katika eneo la Asia-Pasifiki ambao, kama ilivyo kwa Tokyo, wanahusika katika migogoro ya kimaeneo na China.
Mkutano huo wa pande mbili wa mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi unafanyika baada ya gwaride kubwa la kijeshi lililofanywa na China ambalo lilihudhuriwa na viongozi akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kim Jong Un wa Korea Kaskazini.
Wachambuzi wanasema viongozi hao walioalikwa na Rais wa China Xi Jinping ni sehemu ya maono yake kuelekea utaratibu mpya wa uendeshaji wa ulimwengu utakaoiweka kando Marekani.
Japan: Tumekubaliana kuimarisha ushirikiano
Waziri wa Ulinzi wa Japan Gen Nakatani amesema "Tukithibitisha tena umuhimu wa kushirikiana ili kuzuia mabadiliko ya upande mmoja, tumekubaliana kuimarisha ushirikiano." Alisema hayo baada ya mazungumzo yaliyofanyika huko Tokyo.
Shirika la utangazaji la umma la Japan, NHK lilisema nchi hizo mbili zilikubaliana kufanya mafunzo ya hali ya juu ya wanajeshi wao na kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya usalama wa kiuchumi kama vile madini na nishati muhimu.
Mkutano wa Ijumaa unafanyika baada ya Australia kutangaza mpango wa dola za Marekani bilioni 6 mwezi Agosti ili kununua meli za hali ya juu 11 za kivita zilizoundwa na kampuni ya Japan ya Mitsubishi Heavy Industries, katika kile ambacho kimetajwa kuwa mojawapo ya mikataba mikubwa zaidi ya ulinzi kuingiwa na Japan tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Australia inalifanyia mageuzi jeshi katika kukabiliana na China
Australia nayo inafanya mageuzi makubwa ya kijeshi, kuliimarisha jeshi lake la maji na makombora ya masafa marefu, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na China.
Beijing na Tokyo zinakabiliwa na mzozo juu ya visiwa vinavyodhibitiwa na Japan katika Bahari ya China Mashariki na maafisa wa Japan mara kwa mara wanapinga uwepo wa walinzi wa pwani ya China na meli nyingine kwenye maji yanayozunguka visiwa vya pembezoni.
"Pia tumezungumzia wasiwasi wetu kuhusu shughuli zinazovuruga utulivu katika bahari ya Mashariki na Kusini mwa China na kusisitiza msimamo wetu wa muda mrefu wa kupinga mabadiliko yoyote ya upande mmoja," Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong naye aliwaambia waandishi wa habari.