Wafuasi wa Bashir pia wamlaumu Bashir kwa uhalifu.
9 Machi 2009Wakati rais Omar al Bashir wa Sudan anatishia kuyafukuza mashirika zaidi ya misaada kuondoka nchini mwake , wafuasi wake wa hapo awali pia wanamlaumu rais huyo kwa kutenda uhalifu.
Rais al Bashiri ametoa kauli hiyo ya vitisho katika ziara yake ya kwanza kwenye jimbo la Darfur tokea Mahakama ya Kimataifa dhidi ya uhalifu ya mjini the Hague itoe waranti juu ya kumkamata rais huyo.
Rais Bashir pia ametishia kuwafukuza wawakilishi wa kibalozi na majeshi yanayolinda amani.
Mahamaka ya Kimataifa inakusudia kumkamata kiongozi huyo wa Sudan na kumfungulia mashtaka kwa madai ya kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Sudan imeshayafukuza mashirika ya misaada 13 kwa madai kuwa yanashirikiana na Mahakama hiyo ya Kimataifa.
Rais Omar al Bashir alitoa vitisho hivyo katika ziara yake kwenye jimbo la Dafur ambapo alilakiwa kwa shangwe na maalfu ya watu.
Hatahivyo sasa pana ushahidi uliotolewa na watu ambao hapo awali waliorodheshwa na serikali ya Sudan kutenda uhalifu dhidi ya watu wa Darfur.
Shirika moja la Misri linalotetea haki za binadamu limetoa ukanda wa video wenye mahojiano na watu waliokuwa wanamgambo wa Janjaweed waliotumiwa na serikali ya Sudan kutenda uhalifu katika jimbo la Darfur.
Pamekuwapo tuhuma kwamba serikali hiyo iliwatumia wanamgambo hao kufanya mauaji, ubakaji na kampeni ya fagia fagia dhidi ya watu wa Darfur.
Katika ukanda huo wanamgambo hao wanaeleza jinsi walivyofanyakazi kwa niaba ya rais Bashir.
Wamethibitisha madai yaliyotolewa dhidi ya rais huyo.
Mtu mmoja Suleiman aliekuwa mmoja wao ameeleza jinsi makamu wa rais wa Sudan Ali Taha alivyoenda katika mji wa el Fasher na kuwaambiwa kuwa wao ni waarabu.
Makamu wa rais huyo aliahidi kuwapa silaha,fedha, farasi, sare na mahitaji mengine.Makamu wa rais huyo aliwaambia kwamba serikali ya Sudan "inahitaji eneo tu na siyo watu".
Katika ukanda huo wanamgambo wa Janjaweed wa
hapo awali pia wameeleza jinsi walivyokuwa wanabaka wanawake na kutekeleza kampeni ya fagia fagia katika jimbo la Darfur.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu laki tatu wameuawa katika jimbo hilo na mamilioni wengine wamegeuka kuwa wakimbizi. Ni kutokana na madai hayo kwamba Mahakama ya Kimataifa dhidi ya uhalifu ICC ya mjini the Hague imetoa waranti wa kumkamata rais Omar al Bashir na kumfungulia mashtaka.