Jakarta. Waandamanaji wataka wafungwa wauwawe.
12 Oktoba 2005Nchini Indonesia , kiasi cha waandamanaji 500 waliizingira jela moja mapema leo asubuhi , jela ambamo wafungwa watatu walioko katika hukumu ya kifo kuhusiana na shambulio la bomu mjini Bali katika mwaka 2002 wanashikiliwa.
Waandamanaji kadha walipanda katika uzio wa waya na kuvunja mlango wa chuma wa jela ya Kerobokan wakidai kuwa wafungwa hao watatu wauwawe mara moja.
Maafisa wa usalama hata hivyo walikuwa wamewahamishia watu hao watatu katika jela nyingine jana Jumanne, wakieleza kuwa kulikuwa na hali ya wasi wasi wa kiusalama.
Leo ni kumbukumbu ya mwaka wa tatu tangu shambulio hilo dhidi ya club hiyo ya usiku mjini Bali, ambapo watu 202 ikiwa ni pamoja na watalii wengi kutoka Australia waliuwawa. Zaidi ya wanaharakati 30 wamekamatwa na kuhukumiwa kuhusiana na shambulio hilo.