Jaji Mkuu mstaafu David Maraga kugombea urais Kenya
20 Juni 2025Akiwa na umri wa miaka 74, Maraga ambaye alihudumu kwenye wadhfa wa Jaji Mkuu kutoka Oktoba mwaka 2016 hadi alipostaafu Januari mwaka 2021, amejitambulisha kama mgombea wa kizazi cha vijana wa Gen Z, akijaribu kutumia wimbi la kutoridhishwa na utawala wa Rais William Ruto lililoenea miongoni mwa vijana.
Kundi hili ndilo lililoongoza maandamano ya kihistoria ya taifa hilo dhidi ya Mswada wa Fedha mwezi Juni mwaka jana na sasa limegeuka kuwa nguzo muhimu ya kisiasa.
"Inasikitisha mno kuona namna vijana wetu wanavyonyanyaswa. Hatuwezi kuendelea kuwaangalia baadhi ya watu wakichukulia taifa kana kwamba ni mali yao binafsi. Tunahitaji kuchukua hatua. Na kwa sababu hiyo, nimeamua kuwania urais mwaka 2027."
Maraga ametaja uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 kama mapambano kati ya wale wanaoamini katika utawala wa sheria na wale wanaokiuka sheria waziwazi hata kufikia hatua ya kuwaua watoto kama panya. Tangazo la Maraga linamweka katika orodha ya viongozi wanaopanga kuwania kiti hicho dhidi ya Rais Ruto.
Wengine walioonyesha nia hiyo ni kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Taifa Dokta Fred Matiang'i, kiongozi wa PLP Martha Karua na Eugene Wamalwa wa DAP-K.
Ingawa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua aliondolewa madarakani na kupigwa marufuku kugombea, ameashiria kuwa atawania endapo njia ya rufaa itamruhusu.
"Nitafanya kila mmoja kuheshimu sheria"
Maraga anakumbukwa kwa mchango wake katika kupanua demokrasia ya haki na uongozi wake mahakamani alipofanikisha historia mwaka 2017 kwa kuongoza Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa urais kwa msingi wa dosari na ukiukwaji wa kikatiba.
David Maraga amesema hali inayoshuhudiwa nchini kwa sasa ni ya uvunjifu mkubwa wa utawala wa sheria. Walioko mamlakani wanaamini wanaweza kufanya chochote na kutoroka bila kuwajibishwa.
"Iwapo ningepewa fursa ya kuliongoza hili taifa, nitafanya kila mmoja kuheshimu sheria, wanavyofanya kila mtu kuheshimu sheria kila kitu kitaelekea kuwa sawa."
Iwapo ningepewa fursa ya kuliongoza hili taifa, nitafanya kila mmoja kuheshimu sheria. Unapofanya kila mmoja kuheshimu sheria, kila kitu kitaelekea kuwa sawa.”
Aliongeza kuwa alishawahi kupendekeza kuvunjwa kwa Bunge kwa kushindwa kutekeleza sheria ya usawa wa kijinsia na anaamini kuwa hatua kama hizo ndizo zitakazosaidia taifa kurejea kwenye mkondo wa haki.
Je, jaji huyu mstaafu atafanikiwa kuwashawishi wakenya ambao wamezoea kupiga kura kwa misingi ya kikabila kuweka kura zao kwenye kapu moja kwenye uchaguzi mkuu ujao?