Jaji asema wahamiaji wanatendewa vibaya na utawala wa Trump
25 Machi 2025Katika vita vya kisheria vilivyokuwa na mvutano mkubwa, jaji wa shirikisho amekosoa vikali matumizi ya utawala wa Trump ya Sheria ya Maadui wa Wageni ya 1798 (AEA) katika kuwarudisha wahamiaji wa Venezuela wanaoshukiwa kuwa wanachama wa magenge ya kihalifu.
Utata huu umeibuka baada ya utawala wa Rais Donald Trump kutumia sheria hii ya zamani kuwapeleka wahamiaji wawili kutoka Venezuela kwenda gerezani nchini El Salvador mnamo Machi 15, huku mchakato wa kisheria ukiendelea kujadili kuhusu mpaka wa mamlaka ya utawala wa rais, haki za binadamu, na haki ya kupata haki za kisheria.
Machi 15, Rais Trump alitumia Sheria ya Maadui wa Kigeni ya 1798 (AEA), ambayo kawaida hutumika kuwalenga raia wa nchi zinazohusishwa na vita, kuhamisha wahamiaji wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Tren de Aragua (TdA), ambalo linahusishwa na shughuli za kihalifu.
Hatua hii ilisababisha upinzani mkubwa wa kisheria, ambapo Jaji James Boasberg wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani katika jiji la Washington alitoa amri ya kusitisha uhamisho wa wahamiaji chini ya sheria hii kwa muda.
Amri ya mahakama na ukaidi wa utawala wa Trump
Jaji Boasberg alitoa amri ya zuio ya muda ambayo iliizuia serikali ya Trump kusafirisha ndege nyiingine za uhamisho chini ya AEA, na kesi hii sasa inafuatiliwa kwa karibu. Hata hivyo, Wizara ya Sheria ya Marekani inajitahidi kutaka amri hiyo iondolewe, ikisema kuwa amri hiyo inakiuka mamlaka ya Rais katika masuala ya vita na sera za kigeni. Wakili wa Wizara ya Sheria, Drew Ensign, alidai kuwa amri hiyo inavunja mipaka ya mamlaka ya kisheria ya Rais.
Mawakili wa wahamiaji waliohamishwa wamekuwa wakidai kuwa wateja wao hawakuwa wanachama wa kundi la TdA na hawajafanya makosa yoyote ya kihalifu. Walidai kwamba wahamiaji hawa walilengwa tu kwa misingi ya michoro ya tattoo, bila ushahidi wa kutosha. Hii inachochea wasiwasi kuhusu uwezekano wa upendeleo na ubaguzi katika mchakato wa uhamisho, ambapo wahamiaji hawa walinyimwa haki ya kujitetea katika mashauri ya kisheria.
Soma pia: Trump kuandaa kituo cha Guantanamo kwa ajili ya wahamiaji 30,000
Jaji Patricia Millett, ambaye aliteuliwa na Rais Barack Obama, alikosoa vikali hatua hii, akisema kuwa wahamiaji waliokuwa kwenye ndege walinyimwa kabisa fursa ya kupinga uhamisho wao chini ya AEA. Alisema kwamba "Manazi walitendewa bora chini ya Sheria ya Madui wa Kigeni" wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, kwa kuwa walikuwa na nafasi ya kujitetea mbele ya kamati za kusikiliza kabla ya kuhamishwa.
Majadiliano ya kisheria na maoni ya majaji
Katika mjadala wa kisheria, majaji walikuwa na mitazamo tofauti. Jaji Millett alionyesha kutoridhishwa na upande wa serikali, akisisitiza umuhimu wa kutoa haki kwa wahamiaji hawa. Hata hivyo, Jaji Justin Walker, ambaye aliteuliwa na Rais Trump, alikubali wazo la kuwapa wahamiaji haki ya kusikilizwa, ingawa alionekana kuunga mkono zaidi utetezi wa serikali kuhusu mamlaka ya rais.
Upinzani dhidi ya amri hiyo ya kizuizi umejikita katika wasiwasi wa serikali kwamba ikiwa amri hiyo itabatilishwa, uhamisho wa wahamiaji utaendelea mara moja. Lee Gelernt, wakili kutoka Shirikisho la Haki za Raia la Marekani (ACLU), alionya kwamba wahamiaji hao watapelekwa kwenye gereza la El Salvador, ambalo lina sifa ya kuwa mojawapo ya magereza hatari zaidi duniani.
Kesi hii inazungumzia masuala makubwa ya utawala wa sheria na haki za binadamu. Imejenga mjadala kuhusu iwapo utawala wa Trump unapitia mipaka ya kisheria kwa kutumia sheria ya zamani ya AEA kutekeleza mikakati ya uhamisho ya wahamiaji bila kuwapa nafasi ya kujitetea. Hii inawakumbusha wataalamu wa sheria kuhusu umuhimu wa kuheshimu mchakato wa kisheria hata wakati wa mizozo ya kigeni.
Hatima ya kesi na athari zake kisheria
Kesi hii inategemewa kuendelea kuwa na athari kubwa katika historia ya sheria za kimataifa na haki za binadamu. Ikiwa utawala wa Trump utaendelea kupuuza amri ya mahakama, inaweza kuanzisha mzozo wa kikatiba ambao utaathiri uhusiano kati ya mamlaka ya serikali na ile ya mfumo wa kisheria.
Soma pia: Trump aamuru kufungwa kwa muda kituo cha habari cha VOA
Kadhalika, utawala wa Trump unaendelea kuimarisha utekelezaji wa AEA katika mikakati yake ya kudhibiti uhamiaji.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu Todd Blanche, serikali inapanga kuhamisha wanachama wawili wa TdA ambao wanakabiliwa na mashtaka ya utapeli na utekaji nyara kwenda Chile chini ya AEA.
Hata hivyo, mjadala huu bado unaendelea, na wataalamu wengi wa sheria wanashikilia kuwa hili linaweza kuwa ni hatari kwa haki za wahamiaji na utawala wa sheria kwa ujumla.