Israel yazidi kushtumiwa kwa hatua zake dhidi ya Gaza
10 Machi 2025Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Palestina, imesema inalaani vikali uamuzi wa wizara ya nishati ya Israel wa kukata umeme kwenye Ukanda wa Gaza, na kwamba inaichukulia hatua hiyo kuwa ni ya kuongeza matendo ya mauaji ya halaiki, kuchochea janga la wakimbizi wa ndani pamoja na lile la kibinadamu katika ukanda wa Gaza.
Ujerumani yaishtumu Israel kwa kukatiza msaada kwa Gaza
Serikali ya Ujerumani imesema leo kuwa uamuzi huo wa Israel wa kukatiza kusambazwa kwa bidhaa za msaada na umeme kwa Gaza, kunaweza kuchochea mzozo mpya wa kibinadamu katika eneo hilo.
Ujerumani yaihimiza Israel kuondoa vikwazo vya misaada Gaza
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Kathrin Deschauer , amesema Gazakwa mara nyingine tena inatishiwa na uhaba wa chakula na kukatizwa kwa umeme hakukubaliki na hakuambatani na jukumu la Israel chini ya sheria ya kimataifa.
Uingereza pia yaishtumu Israel
Serikali ya Uingereza nayo pia imeitaka Israel kurejesha usambazaji wa umeme huko Gaza, ikionya kuwa nchi hiyo huenda inakiuka sheria za kimataifa.
Msemaji rasmi wa waziri mkuu Keir Starmer, amewaambia waandishi wa habari kwamba wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na ripoti hizo na kuihimiza Israel kuondoa vikwazo hivyo.
Masharika ya UN yahimizwa kujaza nafasi ya UNRWA
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Daniel Meron amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba Israel inafanya kazi kutafuta mbadala wa shirika la UNRWA ndani yaGaza. Hata hivyo hakutoa maelezo ya kina zaidi.
Ujumbe wa Israel waelekea Doha
Ujumbe wa israel umeondoka kuelekea Doha kwa mazungumzo mapya ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza . Haya ni kulingana na afisa mmoja waIsrael aliyeliarifu shirika la habari la AFP.
Chanzo kinachofahamu kuhusu mazungumzo hayo kilichozungumza kwa sharti ya kutotambulishwa, hakikutoa maelezo zaidi.