Israel yawazuia Wapalestina kurejea Kaskazini mwa Gaza
26 Januari 2025Israel imefanya hivyo ikiliishutumu kundi la Hamas kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. Imedai kuwa kundi hilo limebadilisha mtiririko wa mateka liliowaachia, kwa kuwa raia wake bi Arbel Yehoud, alipaswa kuachiliwa huru kabla ya mateka wanajeshi walioachiliwa huru jana Jumamosi.
Soma zaidi: Israel yatishia kuwazuia Wapalestina kurejea kaskazini mwa Gaza
Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya ya Lebanon imesema watu 11 wameuwawa Kusini mwa Lebanon ambako kumezuka mvutano baada ya kumalizika kwa muda wa kusalia majeshi ya Israel katika maeneo hayo.
Wanajeshi hao walipaswa kuondoka kwenye maeneo hayo kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah. Kulingana na Wizara ya Afya ya Lebanon, watu wengine 83 wamejeruhiwa katika mvutano huo wakati wakijaribu kurejea makwao.
Israel imesema, wanajeshi wake wataendelea kubaki Kusini mwa Lebanon kwa sababu Lebanon bado haijatekeleza kikamilifu masharti ya kuacha kuwa na silaha za Hezbollah.