Israel yawashambulia waasi wa Houthi Yemen
28 Mei 2025Waziri huyo wa Ulinzi wa Israel amesema shambulio walilofanya dhidi ya waasi wa Houthi ni ishara na ujumbe wa wazi wa kuendelea na sera yao kwamba mtu yeyote atakaeishambulia Israel atawajibishwa vikali.
Kulingana na jeshi la Israel shambulizi hilo liliharibu ndege moja inayomilikiwa na waasi hao na inayoaminika kutumika kuwasafirisha magaidi, wanaotumiwa kuishambulia Israel. Jeshi hilo kupitia taarifa yake limesema sawa na uwanja wa ndege wa Hodeida na Salif, uwanja wa ndege wa Sanaa unaendeshwa na wahouthi na unatumiwa kuendesha operesheni za kigaidi.
Ujerumani, Finland zashinikiza misaada kuingia Gaza
Shambulio hilo limekuja siku moja baada ya Israel kuripoti kudungua makombora mawili yaliyovurumishwa nchini mwake kutoka Yemen na waasi hao wanaoungwa mkono na Iran. Waasi hao wa Houthi waliokiri kutekeleza shambulio hilo, wamekuwa mara kwa mara wakiishambulia Israel kwa makombora na droni tangu taifa hilo lilipoanzisha vita vyake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas mjini Gaza, mnamo Oktoba mwaka 2023.
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Huku hayo yakiarifiwa Israel imeendeleza mashambulizi yake pia katika Ukanda wa Gaza. Afisa mmoja mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema watu 47 wamejeruhiwa, kufuatia risasi zilizofyatuliwa na wanajeshi wa taifa hilo katika mkusanyiko wa watu kwenye kituo cha kugawa misaada mjini Gaza.
Mamia ya Wapalestina wavamia vituo vya msaada Gaza licha ya hofu ya ukaguzi wa kibayometriki
Maelfu ya wapalestina walionekana wakikimbilia kituo hicho kinachoendeshwa na wakfu wa Israel wa GHF. Ajith Sunghay Mkuu wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, amesema bado wanachunguza kisa hicho kubaini hasa kile kilichotokea. Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yamekataa kufanya kazi na GHF, wakidai inafanya kazi na Israel bila kuwahusisha wajumbe wowote wa Palestina.
Waziri wa nje wa Italia asema Israel lazima ikomeshe mashambulizi yake Gaza
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani, akilihutubia bunge la nchi hiyo ameitolea mwito Israel kuachana na mashambulizi yake Gaza, huku akitoa onyo kwamba kuwafukuza wapalestina katika ardhi yao hakutakubalika. Ameukosoa pia mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka kulidhibiti eneo zima la Ukanda wa Gaza, kwa kuwafurusha wapalestina wanaoishi huko.
"Nataka kusisitiza ndani ya bunge hili kwa uwazi kwamba kuondolewa kwa wapalestina kutoka Gaza hakutakubalika. Ndio maana tunaunga mkono kikamilifu mpango wa mataifa ya kiarabu unaoongozwa na Misri wa kuujenga upya Ukanda huo ambao haufungamanishwi na mpango wowote wa kuwaondoa kwa nguvu wapalestina," alisema Tajani.
Kansela Merz aikosoa Israel kwa inachofanya Gaza
Tajani ameongeza kuwa Mashambulizi ni lazima yakomeshwe na harakati za kutoa misaada ya kiutu zianzishwe mara moja na kuheshimiwa kwa sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu na kutaka pia wanamgambo wa Hamas kuwaachia mateka wote inaowashikilia.
reuters,ap, afp