Israel yawaachia mamia ya wafungwa wa kipalestina
15 Februari 2025Israel imewaachia mamia ya wafungwa wa kipalestina baada ya kundi la Hamas kuwaachia mateka watatu wa Israel mapema leo Jumamosi kama kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza. Hayo yamethibitishwa na maafisa wa Palestina.
Picha na video zimeyaonesha mabasi manne yaliyowabeba wafungwa hao yakifika katika eneo la ukingo wa magharibi na kulakiwa na wapendwa wao. Katika awamu ya sasa, Hamas ilitakiwa kuwakabidhi mateka watatu wa Israel kwa mabadilishano na wafungwa 369 wa Kipalestina kutoka jela za Israel.
Soma zaidi: Hamas na Israel wabadilishana tena wafungwa na mateka
Mabadilishano hayo yalikuwa mashakani mapema wiki hii kufuatia tangazo la Hamas la kuchelewesha kwa muda kuwaachia huru mateka zaidi wa Israel, ikiituhumu nchi hiyo kukiuka vipengele vya mkataba wa kusitisha mapigano kwa siku 42 lakini mazungumzo ya dakika za mwisho yamefanikisha kukamilika kwa mpango huo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, anatarajiwa kuitembelea Israel leo kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu makubaliano ya usitishaji vita kwenye Ukanda wa Gaza.