Vyombo vya habari vyachochea chuki dhidi ya Wayahudi
3 Juni 2025Mwanadiploamasia huyo wa ngazi za juu wa Israel ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa X kwamba ameshtushwa na shambulizi hilo baya kabisa la kigaidi na chuki dhidi ya Wayahudi, lililowalenga Wayahudi waliopo Boulder, Colorado nchini Marekani.
Ameandika, kitendo hicho ni chuki ya wazi dhidi ya Wayahudi, kilichochochewa na kauli za chuki zinazowachukulia Wayahudi kama waumiani, ikimaanisha wanamwaga na kutumia damu ya watu wengine kwenye ibada zao, shutuma ambazo amedai zinasambazwa na vyombo vya habari. Hata hivyo hakufafanua zaidi kuhusu madai haya.
Mtu mmoja aliwarushia vilipuzi waandamaji hao na watu wanane walijeruhiwa vibaya kwa moto.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa upande wake amesema anatumai mamlaka za Marekani zitamshughulikia kikamilifu mshambuliaji huyo kwa kuzingatia sheria za nchini humo.
Netanyahu ataka dhana inayochochea chuki kuachwa mara moja
Kulingana na taarifa kutoka kwenye ofisi yake, kiongozi huyo amesema mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi kote ulimwenguni yanatokana na shutuma hizohizo za kiimani dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi pamoja na watu wake.
Chanzo cha dhana hiyo ya kiimani ni tukio lililochochea Yesu Kristo kuuawa chini ya utawala wa Kirumi. Na Wakristu hasa barani Ulaya waliamini kwamba Mayahudi walikuwa wakiwaua Wakristo na kutumia damu yao kwa matambiko na ibada zao nyingine. Netanyahu amekemea na kutaka dhana hiyo kuachwa mara moja.
Mshambuliaji huyo alisikika akipiga kelele "Uhuru kwa Palestina!!" na kisha kuwarushia waandamanaji vilipuzi hivyo.
Idara ya Upelelezi wa ndani nchini Marekani, FBI imelitaja shambulizi hilo kuwa ni la kigaidi. Afisa maalumu anayehusika na Ofisi ya Upelelezi ya Denver Mark Michelek amesema upelelezi wa awali unaonyesha dhahiri kwamba kitendo hicho kililenga kuleta machafuko na FBI inakichunguza kama shambulizi la kigaidi.
Mkuu wa Polisi wa Boulder, Stephen Redfearn kwa upande wake ameomba watu kuwa wavumilivu wakati polisi wakiendelea na uchunguzi. Alisema "Ninaomba kuwepo na uvumilivu, wakati tunaendelea na hili. Lakini pia ninaomba muungane pamoja nami katika kuwakumbuka wahanga, familia na kila mmoja aliyeathirika kwenye janga hili. Na tutafanya kila liwezekanalo ili kutoa majibu kwa wote."
Ni shambulizi linalofanywa siku chache baada ya wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israel kuuawa kwa kupigwa risasi huko Washington.
Na huko Gaza, karibu watu 31 wameuawa na zaidi ya 170 kujeruhiwa, baada ya vikosi vya Israel kulishambulia kundi kubwa la watu waliokuwa wakienda kuchukua msaada wa chakula, maafisa wa afya na mashuhuda wamesema.
IDF ilifanya mashambulizi hayo karibu kabisa na kituo inachokisimamia cha kugawa misaada. Hata hivyo, Israel yenyewe imekana kuwashambulia raia hao.