Israel yauwa 80 wakisaka chakula Gaza
21 Julai 2025Kupitia mtandao wa X, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) liliandika kwamba idadi kubwa ya watu wenye njaa waliuawa siku ya Jumapili (Julai 20), muda mfupi baada ya magari 25 ya shirika hilo kuvuuka mpaka wa Zikim na kuingia Gaza.
"Wakati msafara huo unawasili, watu waliokuwa wameuzunguka walishambuliwa na vifaru, wadunguaji na aina nyengine za silaha, ambapo idadi ya watu isiyojulikana waliuawa na kujeruhiwa." Ilisema taarifa hiyo.
Wizara ya Afya ya Gaza ilisema watu waliouawa ni 80na wengine 60 walijeruhiwa katika tukio hilo ambalo si la mwanzo kutokea, huku WFP ikisema kwamba "watu hawa walikuwa wanajaribu tu kukifikia chakula cha kuzilisha familia zao ilhali wakiwa kwenye ukingo wa kufa kwa njaa."
Jeshi la Israel lilidai vikosi vyake vilirusha risasi za tahadhari kutokana na kile lilichokiita "kitisho cha ghafla"
Hata hivyo, jeshi hili liliezea wasiwasi wake juu ya idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa, ingawa liliahidi kuyachunguza mazingira ya tukio lenyewe.
Shirika la habari la Palestina (WAFA) lilivinukuu vyanzo mbalimbali vya kitabibu vikisema kwamba watu 132 walikuwa wameuawa kwenye Ukanda wa Gaza, 94 kati yao wakiwa wasakaji misaada, tangu siku Jumapili.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mamia ya watu wameshauawa wakiwa kwenye maeneo ya kugawa chakula au karibu na magari ya misaada tangu mwezi Mei.
Israel yaishambulia tena Yemen
Siku ya Jumatatu (Julai 21) Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema jeshi la nchi yake liliyashambulia yale aliyoyaita "maeneo ya magaidi" katika bandari ya Hodeida nchini Yemen.
"Jeshi letu limeshambulia maeneo ya kigaidi ya utawala wa kigaidi wa Wahouthi kwenye bandari ya Hodeida, na linahakikisha linazuwia jaribio lolote la magaidi hao kurejelea mashambulizi yao dhidi ya miundombinu yetu." Ilisema taarifa iliyotolewa na waziri huyo wa ulinzi.
Shirika la habari la AFP lilimnukuu afisa mmoja wa serikali ya Wahouthi akikiri kufanyika kwa mashambulizi hayo, ingawa alisisitiza kuwa kilichoshambulia hasa "ilikuwa gati ambayo ilikuwa imejengwa upya baada ya kuharibiwa na Israel siku za nyuma."
Jeshi la Ansarullah, wengine wanawaita Wahouthi, limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Israel kwa kile linachodai ni kuwaunga mkono Wapalestina wanaoshambuliwa kila siku na jeshi la Israel.
Jeshi hilo limeapa kuendelea na kampeni yake hiyo inayojumuisha mzingiro kwenye Bahari ya Sham dhidi ya meli zinazohusishwa na Israel, hadi pale Tel Aviv itakapokomesha vita vyake dhidi ya Gaza.