Israel yaua 5 Gaza wakiwemo wanahabari wa Aljazeera
11 Agosti 2025Jeshi la Israel limethibitisha kifo cha Anas al-Sharif kupitia mitandao ya kijamii, likimtuhumu kuwa kiongozi wa seli ya kigaidi ya kundi la Hamas, huku akijifanya kuwa mwandishi wa habari.
Jeshi hilo lilitaja taarifa za kiintelijensia na nyaraka zilizopatikana Gaza, zikiwemo orodha za wanachama, orodha za mafunzo ya kigaidi, na rekodi za mishahara, kama ushahidi wa ushiriki wa al-Sharif katika kupanga mashambulizi ya roketi dhidi ya raia na wanajeshi wa Israel.
Al Jazeera ilikanusha madai ya Israel, ikisema hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa na kuthibitishwa kwa njia huru.
Wengine waliouawa ni Mohammed Qreiqeh na wapiga picha watatu.
Kulingana na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (Committee to Protect Journalists), waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari wapatao 230 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo wa Gaza miezi 22 iliyopita.