Israel yatishia kuwazuia raia kurejea kaskazini mwa Gaza
25 Januari 2025Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema ni lazima mateka huyo Arbel Yehud ambaye ni raia wa kawaida aachiwe kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya makubaliano na Hamas.
Katika taarifa yake, kundi la Hamas limesema mateka huyo bado yupo hai na mwenye afya njema, lakini haijafahamika iwapo itamwachia huru leo Jumamosi kama ilivyotarajiwa. Hamas iliwaachilia siku ya Jumamosi hii mateka wanne ambao ni wanajeshi wa kike huku Israel ikiwaachilia huru wafungwa 200 wa Kipalestina.
Baada ya hapo, Israel inatarajiwa kuanza kuondoa vikosi vyake kutoka kwenye ujia wa Netzarim unaoitenganisha Gaza pande mbili.
Hatua itakayoruhusu Wapalestina walioamriwa na Israel kuhamia kusini mwa ukanda huo kuanza kurejea kwa mara ya kwanza katika eneo la kaskazini mwa Gaza tangu kuanza kwa vita.