Israel yatishia kuchukua udhibiti wa eneo lote la Gaza
19 Mei 2025Israel imetangaza kuwa itaruhusu usambazaji mdogo wa misaada ya kibinaadamu kwa Wapalestina wanaokabiliwa na hali ngumu katika Ukanda wa Gaza wakati mashambulizi yakiendelea kusababisha vifo.
Mamlaka za Gaza zimesema karibu watu 103 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa sehemu mbalimbali huko Gaza kuanzia Jumapili na mapema Jumatatu asubuhi kufuatia mashambulizi makali ya Israel ambayo yamepelekea pia kufungwa kwa hospitali kubwa kaskazini mwa Gaza.
Israel inadai kuwa wimbi hili jipya la mashambulizi ni la kuishinikiza Hamas kukubali mpango wa kusitisha mapigano kwa muda na kuachiliwa kwa mateka, lakini kundi hilo la Kipalestina linasisitiza kuwepo mpango wa kumaliza kabisa vita na kuondolewa kwa majeshi ya Israel huko Gaza.
Ukosoaji wa kimataifa umeongezeka dhidi ya Israel ikitakiwa kusitisha vita huko Gaza. Siku ya Jumamosi, viongozi wa nchi za Kiarabu walilaani harakati za Israel na kutoa wito wa usitishwaji mara moja mapigano.
Siku ya Jumapili, Wabunge wa Italia waliandamana kwenye mpaka wa Gaza upande wa Misri ili kupinga vita hivyo. Cecilia Strada ni mmoja wao ambaye pia ni mbunge wa bunge la Ulaya:
"Ulaya inapaswa kuchukua hatua zaidi. Kwa sasa haifanyi chochote kuzuia mauaji haya. Ulaya inapaswa kutumia uwezo wote ilionao kukomesha yote haya. Nadhani kunapaswa kuwepo vikwazo kamili vya silaha kwenda na kutoka Israel, na pia kusitisha biashara na maeneo haramu ya walowezi."
Israel kuruhusu misaada kuingia Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza siku ya Jumapili uamuzi wa kusitisha mzingiro wa Gaza na kuruhusu kuingia na kusambazwa kwa idadi ndogo ya misaada ya kibinaadamu akisema kuwa Israel imechukua uamuzi huo kutokana na sababu za kidiplomasia ili kuzuia janga la njaa kwa raia wa Gaza, akiongeza kuwa hata marafiki wa Israel wasingelivumilia kushuhudia baa la njaa likilikumba eneo hilo.
Hata hivyo, Netanyahu alisema Israel itaendeleza operesheni zake za kijeshi bila kuzuiwa na kwamba watachukua udhibiti kamili wa eneo lote la Gaza ili kuwazuia wapiganaji wa Hamas wasiweze kupora misaada hiyo na kuitumia kwa maslahi yao. Tangu mwezi Machi, Israel ilizuia bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na mafuta, chakula na dawa kuingia Gaza kwa madai kwamba ni kuzidisha mbinyo kwa kundi la Hamas huko Gaza.
Afisa wa Umoja wa Mataifa amesema kwa sasa karibu malori 20 ya misaada yaliyosheheni chakula yapo katika mji wa Arish nchini Misri yakisubiri kuruhusiwa hivi leo kuingia Gaza. Mashirika kadhaa ya misaada yamepongeza uamuzi wa Netanyahu na kuutaja kuwa hatua ya kwanza muhimu katika kuokoa maisha ya Wapalestina zaidi ya milioni 2 wanaoishi katika mazingira magumu.
(Vyanzo: Mashirika)