Israel yatanua mashambulizi ya ardhini kaskazini mwa Gaza
4 Aprili 2025Kulingana na taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa kupitia jukwaa la Telegram kufikia sasa limeshaanza operesheni zake katika kitongoji cha Shejaiya.
Imeongeza kuwa tayari vikosi vya jeshi hilo vimeshawauwa wale lililowataja kuwa ni magaidi kadhaa na vimesambaratisha miundombinu ya kundi la Hamas iliyokuwa ikitumika kupanga na kufanya mashambulizi. Jeshi hilo limesema liliwaruhusu raia kuondoka kwenye eneo hilo kabla na wakati wa shambulio hilo.
Soma zaidi: Israel inatanua operesheni Gaza ili kuteka 'maeneo makubwa'
Kufuatia operesheni hiyo mamlaka za Gaza zimesema operesheni hizo za kijeshi zilizoanza mapema alfajiri zimewauwa watu wasiopungua 30. Taarifa hiyo imesema ni dhahiri idadi hiyo itaongezeka.
Hayo yanaendelea wakati kundi la wanamgambo wa Hamas likisema kuwa wanachama wake wawili wameuwawa katika shambulio lililofanywa na jeshi la Israel katika mji wa Sidon nchini Lebanon.
Katika taarifa iliyotolewa na tawi la kijeshi la kundi hilo la Al-Qassam limemtaja kamanda wake Hassan Farhat kuwa ni mmoja wa waliouwawa pamoja na watoto wake wawili, wakike na wakiume. Mtoto wake wa kiume alikuwa pia mwanachama wa kundi hilo.
Turk ataka mauaji ya wahudumu wa afya na misaada ya kiutu yachunguzwe
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametaka uchunguzi huru ufanyike baada ya wahudumu wa afya na wafanyakazi wa misaada ya kiutu kuuwawa hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza.
Amesema ameshtushwa na mauaji hayo ya wafanyakazi 15 wa huduma za afya na wafanyakazi wa misaada ya kiutu, suala linaloongeza wasiwasi juu ya uhalifu wa kivita unaofanywa na jeshi la Israel.
Amesisitiza kuwa, ni lazima kuwe na uchunguzi huru, wa kina na wa haraka juu ya mauaji hayo na wote waliohusika kukiuka sheria ya kimataifa kwa namna yoyote hawana budi kuwajibishwa.
Türk ametoa wito wa kusitishwa kwa vita na kuingizwa kwa misaada bila ya vikwazo katika ukanda huo. Ameonya pia kuwa kuna hatari kubwa inayoongezeka kwamba uhalifu wa kikatili unaendelea kufanyika Palestina.