Israel yatakiwa kusitisha mpango wake wa kuidhibiti Gaza
8 Agosti 2025Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliliomba Baraza lake la Usalama kuupitisha mpango wake huo wa kuukalia kimabavu mji wa Gaza, licha ya kuonywa na maafisa wakuu wa kijeshi dhidi ya hatua hiyo.
Israel imesema itauchukua Mji huo, wakati ambapo vita vyake katika Ukanda wa Gaza vinaongezeka. Uamuzi huu wa Israel umefikiwa baada ya saa kadhaa za mkutano wa baraza la mawaziri la Israeli uliomalizika mapema asubuhi ya Ijumaa.
Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imesema jeshi la nchi hiyo linajiandaa kuudhibiti mji wa Gaza na kwamba litawapa msaada wa kibinadamu Wapalestina walio nje ya maeneo ya mapigano.
Uamuzi huu wa Israel unakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa inayoitaka Israel kuvikomesha vita, na wakati huo huo serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu inashinikizwa pia ndani ya Israel, ambako maafisa wa kijeshi wa zamani wamesisitiza kwamba hakuna faida ya kuendeleza vita katika Ukanda wa Gaza ambavyo vitahatarisha maisha ya mateka, takriban 20 wanaozuiliwa Gaza na ambapo baadhi yao wanaaminika kuwa bado wako hai.
Umoja wa Mataifa
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, amesema "mpango wa Serikali ya Israel wa kuutwaa kabisa Ukanda wa Gaza unaokaliwa kwa mabavu lazima usitishwe mara moja". Amesisitiza wajibu wa serikali zote kuishinikiza Israel kukomesha mauaji, kuhakikisha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu, na kuzingatia haki za binadamu.
Turk, amekariri wito wa kusitisha mapigano kabisa, kuachiliwa kwa mateka, na upatikanaji wa misaada bila vikwazo. Amesisitiza haja ya haki, uwajibikaji, na msaada kwa ajili ya ujenzi wa Palestina unaozingatia haki za binadamu.
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameongeza kuwa vivyo hivyo Israel inapaswa kuwaachia huru "Wapalestina wanaozuiliwa kiholela ".
Kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid, ameuelezea uamuzi wa Baraza la Mawaziri la Usalama la Israel kuwa ni "janga" litakalosababisha maafa makubwa zaidi." Amesema hatua iliyopangwa ya kuutwaa mji mkubwa katika Ukanda wa Gaza inaweza kusababisha vifo vya mateka pamoja na kuuawa wanajeshi wengi wa Israel.
Lapid amesema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, anaongozwa na washirika wake wa mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich ambao ni mawaziri katika muungano wa serikali yake.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, amesema uamuzi wa Israel sio sahihi na ameitaka serikali ya Israel kufikiria upya. Amesema hatua ya Israel haitasaidia chochote katika kukomesha mgogoro wa Gaza au kusaidia kuachiliwa kwa mateka bali itaongeza tu umwagaji damu.
Uturuki kwa upande wake imeitaka jumuiya ya kimataifa kuuzuia mpango wa Israel wa kuudhibiti mji wa Gaza, imesema hatua hiyo ni "pigo zito" kwa amani na usalama.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutimiza wajibu wake ili kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi huo ambao unalenga kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao.
Vyanzo: DPA/AFP