Israel yatakiwa kuachana na mpango wa kuiteka Gaza
29 Agosti 2025Akizungumza Alhamisi na waandishi habari, Guterres amesema maelfu ya raia wa Gaza watalazimika kukimbia tena, na kuzitumbukiza familia katika hatari kubwa zaidi. Amerudia wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja, akisema tangazo la Israel kuhusu nia yake ya kuudhibiti Mji wa Gaza, linaashiria hali mpya ya hatari na kutoa wito wa kuwepo upatikanaji wa misaada ya kiutu.
''Hakuna suluhisho la kijeshi katika mzozo huu. Njaa ya raia haipaswi kamwe kutumika kama silaha ya kivita. Raia lazima kulindwa. Usambazaji wa misaada ya kiraia usikwamishwe. Natoa wito kwa mara nyingine wa kusitishwa mara moja mapigano, kuwepo upatikanaji wa misaada ya kiutu Gaza, na kuachiliwa mara moja mateka wote na bila masharti,'' alisisitiza Guterres.
Maandalizi ya mpango wa kuwahamisha watu Gaza yanaendelea
Siku ya Jumatano, msemaji wa jeshi la Israel alitangaza kwamba maandalizi yalikuwa yanaendelea kwa ajili ya mpango wa kuwahamisha wakaazi wa Gaza, mji ambao unasadikiwa kukaliwa na takribani watu milioni 1. Idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni mbili wa Gaza wameyakimbia makaazi yao wakati wa vita.
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich ameitaka serikali ya nchi hiyo kuanza kujinyakulia sehemu ya maeneo ya Ukanda wa Gaza, iwapo kundi la wanamgambo la Kipalestina la Hamas, litaendeleza msimamo wake wa kukataa kuweka chini silaha. Smotrich ambaye amekuwa akipinga vikali kufikia makubaliano ya kumaliza mapigano na Hamas, amewasilisha pendekezo lake la ''ushindi wa Gaza ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025'' katika mkutano na waandishi habari mjini Jerusalem, siku ya Alhamisi.
Kulingana na pendekezo la Smotrich, Hamas itapewa muda wa mwisho wa kujisalimisha, kupokonywa silaha na kuwaachia huru mateka wote ambao bado inawashikilia Gaza tangu kundi hilo lilipofanya mashambulizi Oktoba 2023. Amesema ikiwa Hamas watakataa, Israel inapaswa kujitwalia sehemu ya eneo la Gaza kila wiki kwa muda wa wiki nne, na kuifanya sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza kuwa chini ya udhibiti kamili wa Israel.
Waziri huyo anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia, amesema Wapalestina wataambiwa kwanza wahamie kusini mwa Gaza, na kufuatiwa na Israel kulizingira eneo la kaskazini na kati kwa lengo la kuwasambaratisha wapiganaji wowote wa Hamas ambao bado wamebakia huko, na kisha kulinyakua kabisa eneo hilo. Amesema hilo linaweza kufikiwa ndani ya miezi mitatu hadi minne. Aidha, amemtaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuupitisha mpango huo mara moja na kikamilifu.
Turk atakiwa kuyaita mapigano ya Gaza mauaji ya kimbari
Huku hayo yakijiri, mamia ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa umoja huo, Volker Turk, wamemuandikia barua kumtaka aeleza kwa uwazi kuhusu vita vya Gaza kama mauaji ya kimbari yanayoendelea.
Kulingana na barua hiyo iliyotumwa Jumatano na ambayo shirika la habari la Reuters limefanikiwa kuiona, wafanyakazi hao wamesema vigezo vya kisheria vya mauaji ya kimbari kwenye vita hivyo kati ya Israel na Hamas huko Gaza vimefikiwa kutokana na kuangazia ukubwa wake, upeo na asili ya ukiukaji ulioripotiwa huko.
Barua hiyo iliyosainiwa na Baraza la Wafanyakazi kwa niaba ya zaidi ya wafanyakazi 500, imeeleza kuwa ofisi hiyo ina jukumu kubwa la kisheria na kimaadili kukemea vitendo vya mauaji ya kimbari. Iliongeza kuwa, kushindwa kukemea mauaji ya kimbari yanayotokea, kunaondoa na kudhoofisha uaminifu wa Umoja wa Mataifa na mfumo wenyewe wa haki za binaadamu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema haijibu barua za wafanyakazi wa ndani wa Umoja wa Mataifa, hata ikiwa ni za uwongo, zisizo na msingi na zilizotawaliwa na chuki kubwa dhidi ya Israel.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Cindy McCain amesema kuna ''kila ushahidi'' unaoonesha kwamba hakuna chakula cha kutosha katika ardhi ya Palestina.
Soma zaidi: Baa la njaa ni nini hasa?
Akizungumza Alhamisi, McCain amesema wakati wa ziara yake Gaza wiki hii amelishuhudia hilo na kwamba alizungumzia pia na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu hitaji la dharura la misaada zaidi.
McCain ameliambia shirika la habari la AP kwamba njaa inaendelea katika Ukanda wa Gaza. ''Binafsi nilikutana na akina mama na watoto waliokuwa na njaa huko Gaza,'' alifafanua mkuu huyo wa shirika la WFP.
(AFP, DPA, AP, Reuters)