Israel yasitisha vita kwa muda Ukanda wa Gaza
27 Julai 2025Jeshi la Israel limeanza leo Jumapili kutekeleza usitishaji vita kwa muda katika maeneo matatu ya Gaza yenye idadi kubwa ya wakaazi, kama sehemu ya mfululizo wa hatua zilizoanzishwa kufuatia wasiwasi wa kimataifa kuhusu kuongezeka kwa baa la njaa.
Jeshi la Israel litasitisha mashambulio kwa kipindi cha saa 10 kwa siku katika maeneo ya Gaza City, Deir al Balah na Mawasi ili kutowa nafasi ya kile Israel imekiita hatua za kuongeza misaada ya kibinadamu kwenye maeneo hayo yanayokaliwa na watu wengi.
Soma pia: Zaidi ya mashirika 100 ya misaada yatahadharisha kuhusu njaa inayoenea GazaWimbi la kimataifa la ukosoaji wa Israel limeongezeka katika siku za hivi karibuni kufuatia picha zinazoonesha watoto wanavyohangaika kwa madhila na baa la njaa katika Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya jeshi la Israel.
Limesema jeshi hilo kwamba litatenga njia salama za kuingiza msaada kwenye Ukanda huo lakini pia limedondosha chakula kwa kutumia ndege ikiwemo unga,sukari na vyakula vya makopo.
Tahadhari kuhusu kuongezeka kwa njaa Gaza
Kwa miezi sasa wataalamu wa chakula wamekuwa wakitahadharisha juu ya kitisho cha njaa huko Gaza ambako Israel imezuia msaada kuingizwa ikitowa sababu kwamba kundi la Hamas limekuwa likitwaa msaada unaoingia kuimarisha utawala wake.
Israel lakini haikutowa ushahidi wa madai yake hayo. Nchi hiyo imekosolewa ikiwemo hata na mataifa washirika wake wa karibu ambao wanaishinikiza ikomeshe vita vyake hivyo na janga la kibinadamu ililosababisha.
Pamoja na hayo Israel imesema hatua zake hizi mpya zinachukuliwa huku pia ikiendelea na operesheni ya kuwashambulia Hamas katika maeneo mengine ya Gaza.
Muda mfupi kabla ya kuanza usitishaji vita, maafisa wa afya katika Ukanda wa Gaza wameripoti kwamba takriban Wapalestina 16 wameuwawa katika mashambulizi mawili tofauti.
Ripoti nyingine zimeleeza kwamba malori ya misaada imeanza kuonekana ikiingia katika Ukanda wa Gaza kutoka Misri siku ya Jumapili.Soma pia: Mashirika ya habari ya kimataifa yaitaka Israel kuwaruhusu kuingia Gaza
Picha za video za shirika la habari la AFP zimeonesha malori hayo yakiwa katika eneo la mpaka wa kuingia Gaza lakini pia shirika la habari linalofungamanishwa na serikali ya Misri awali lilithibitisha juu ya kuweko misafara hiyo, ikionesha pia video za malori kwenye eneo la kivuko cha Rafah.
Hata hivyo ikumbukwe kwamba malori yanayovuka mpaka wa Rafah hayawezi kuingia moja kwa moja Ukanda wa Gaza kwasababu upande wa Palestina wa mpaka huo ulizingirwa na jeshi la Israel mwaka jana na kuharibiwa vibaya.
Kwa maana hiyo malori yanatakiwa kuzunguuka kilomita chache hadi kivuko cha Karem Shalom ambacho kinadhibitiwa na Israel ambako ukaguzi mkubwa unafanyika kabla ya malori kuruhusiwa kuingia Kusini mwa Gaza.
Umoja wa Mataifa umesema utafanya kile uwezalo kuwafikia watu wanaokabiliwa na njaa katika Ukanda wa Gaza.