Israel yashambulia katika Ukingo wa Magharibi
26 Agosti 2025
Jeshi la Israel limefanya mashambulio katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah hivi leo na kuwajeruhi watu 14 na kufanya uharibifu kwenye mji huo.
Hayo yameelezwa na shirika la Hilali Nyekundu huku ikielezwa kwamba bado kuna hali ya wasiwasi mkubwa katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu, tangu shambulio la Oktoba 2023 lililofanywa na Hamas dhidi ya Israel.
Shirika la Hilali Nyekundu limesema watu saba wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi katika tukio hilo la leo, huku wanajeshi wa Israel wakizuia timu ya shirika hilo kuwafikia waliojeruhiwa kwenye eneo hilo walilolizingira.
Jeshi la Israel limethibitisha kuanzisha operesheni katika Ukingo wa Magharibi japo halikutowa ufafanuzi zaidi. Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani wa Israel, Yair Lapid, ameitolea mwito serikali kufikia makubaliano na Hamas kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza na kufanikisha kuachiliwa huru kwa mateka waliobakia.