Israel yashambulia maeneo ya kijeshi ya Iran
23 Juni 2025Jeshi hilo limesema kwamba zaidi ya ndege 15 za kivita zilishambulia eneo la Kerman-shah na kuyaharibu maeneo hayo pamoja na ghala la kuhifadhi silaha zinazotumika kuishambulia Israel.
Taarifa kutoka ndani ya Iran kwenyewe zinasema mashambulizi ya Israel yamepiga karibu na jengo linalotumiwa na shirika la misaada ya kiutu la Hilali Nyekundu kaskazini mwa mji mkuu, Tehran, na pia kinu cha nyuklia cha Fordow, kilichokuwa kimeshambuliwa na Marekani siku ya Jumamosi (21.06.2025).
Netanyahu: Tutashambulia kila eneo la Iran
Iran kwa upande wake imefanya mkururo wa mashambulizi asubuhi ya leo ndani ya Israel, ikisema imelenga maeneo ya kijeshi na kimkakati yanayotumika kuishambulia.
Israel ilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi nchini Iran mnamo Juni 13 ikidai kuwa inalenga kuizuwia Jamhuri hiyo ya Kiislamu isiwe na silaha za nyuklia. Mashambulizi hayo yameuwa viongozi wa kijeshi, wanasayansi, raia na kuharibu miundo mbinu ya nishati.