Shambulizi la Israel lauwa tabibu Gaza, tisa wajeruhiwa
16 Aprili 2025Shambulio la angani la Israel limepiga lango la Hospitali ya Kuwaiti katika eneo la Muwasi, Gaza, likisababisha kifo cha mhudumu wa afya na kuwajeruhi wengine tisa, wakiwemo wagonjwa waliokuwa wakitibiwa. Hospitali hiyo iko katika eneo linalohifadhi maelfu waliokimbia mapigano.
Wakati huo huo Hamas imedai kupoteza mawasiliano na walinzi wa mateka wa Israeli-Marekani, Edan Alexander, baada ya eneo walilokuwamo kushambuliwa. Katika mazungumzo na Rais Macron wa Ufaransa, Netanyahu amesisitiza kupinga kuundwa kwa taifa la Palestina, akidai kuwa ni "zawadi kwa ugaidi."
Wakati mashambulizi dhidi ya hospitali yakiendelea, Israel imekuwa ikidai kuwa Hamas hutumia vituo vya afya kwa shughuli za kijeshi, lakini wahudumu wa afya wamesema madai hayo hayana msingi. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, watu zaidi ya 51,000 wamepoteza maisha, huku makumi ya maelfu wakiendelea kukimbia mashambulizi.
Vita hivyo vilianza Oktoba 7, 2023, baada ya Hamas kushambulia Israel na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka zaidi ya 250. Idadi ya mateka waliobaki Gaza ni 59, huku 24 wakiaminika bado kuwa hai.