Israel yashambulia kambi ya kijeshi magharibi mwa Tehran
16 Juni 2025Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, Fars, vishindo vya miripuko mikubwa imesikika katika mji mkuu wa Tehran, kufuatia mashambulizi ya mchana wa leo yaliyofanywa na jeshi la Israel dhidi ya kituo kimoja cha kijeshi magharibi mwa mji huo.
Jeshi la Israel linadai kwamba limefanikiwa kuiharibu miundombinu ya kijeshi ya Iran na sasa ndege zake zinaweza kuruka zipendavyo juu ya anga la Jamhuri hiyo ya Kiislamu na kufanya mashambulizi kwenye maeneo mbalimbali. Bado hakujawa na taarifa za madhara ya mashambulizi ya hivi punde ya Israel, lakini kwa siku nne mfululizo pande hizo mbili zimekuwa zikishambuliana na kuharibu maeneo mbalimbali yakiwemo ya kijeshi, miundombinu ya nishati na hata makaazi ya raia.
Israel yaapa kujibu vikali shambulizi la Iran dhidi yake
Israel inadai kuwa imeshaiharibu robo moja ya maeneo ya kurushia makombora ya Iran na vituo kumi vya kamandi za kijeshi vinavyoendeshwa na kikosi maalum cha walinzi wa mapinduzi, Quds.
Iran nayo imetangaza kuendelea kurusha makombora zaidi ya 100 kuelekea Israel ikiapa kuendelea kuishambulia nchi hiyo baada ya Israel kuanza kuishambulia siku ya Ijumaa na kusababisha mauaji ya zaidi ya watu 200 hadi sasa.
Wanaharakati wa Iran wataka mashambulizi kusitishwa mara moja
Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee, amesema kombora moja lilianguka karibu na ubalozi wake, na kusababisha uharibifu mdogo kwa jengo hilo lakini hakuna majeruhi wowote walioripotiwa. Iran kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje Abbas Araghchi imesema itaacha mashambulizi yake pale Israel itakapoacha pia kuishambulia.
Iran: Tutasitisha mashambulizi Israel itakapoacha uchokozi
Huku hayo yakiarifiwa wanaharakati mashuhuri na watengeneza filamu nchini Iran, wametoa wito wa kusitishwa mgogoro kati ya Iran na Israel, wakiitaka Jamhuri hiyo ya Kiislamu kusitisha mvutano uliopo kwa kuacha urutubishaji wa madini yake ya urani.
Wakizungumza na gazeti la Ufaransa la Le Monde, wametaka pia nchi zote mbili kuacha kushambulia maeneo ya miundombinu na kuwaangamiza raia wasiokuwa na hatia.
Wanaharakati hao ni pamoja na washindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Shirin Ebadi na Narges Mohammadi, pamoja na mshindi wa tuzo ya filamu ya Cannes 2025, Jafar Panahi na Mohammad Rassoulof.
Netanyahu: Tutashambulia kila eneo la Iran
Ujerumani yajadili namna ya kuwaondoa raia wake Israel
Kwengineko serikali ya Ujerumani inajadili namna ya kuwaondoa raia wake kutoka Israel kufuatia mzozo huo unaoendelea. Baada ya mataifa ya Ulaya ikiwemo Poland na Jamhuri ya Czech kuanza kuondoa raia wake Israel, msemaji wa ofisi ya mambo ya nje ya Ujerumani mjini Berlin amewataka Wajerumani kujisajili katika orodha ya kujilinda na migogoro inayowasajili Wajerumani walioko nje ya nchi.
Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika eneo zima la Mashariki ya Kati baada ya Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran siku ya Ijumaa ikidai kutaka kuizuwia kuendelea na mpango wake wa nyuklia.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema anatumai mkutano wa viongozi wa G7 nchini Canada, utafikia makubaliano ya kusaidia kusuluhisha mzozo kati ya Israel na Iran, ili kuzuwia kitisho kikubwa cha usalama katika kanda ya Mashariki ya Kati
Reuters, ap,afp