Israel yashambulia jengo la hospitali kuu Gaza
13 Aprili 2025Maafisa wa afya katika Hospitali ya Al-Ahli Arab Baptist wamethibitisha kutokea kwa shambulio hilo, na kusema kwamba iliwahamisha wagonjwa katika jengo lililolengwa baada ya kupokea simu ya tahadhari juu ya shambulio hilo. Hadi sasa hakuna vifo ambavyo vimeripotiwa wala majeruhi.
Katika taarifa yake, jeshi la Israel limesema kwamba lilichukua hatua ya kupunguza madhara kwa raia kabla ya kushambulia jengo hilo ambalo wanasema lilitumiwa na wapiganaji wa Hamas kupanga mashambulizi.
Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi Gaza na lebanon
Wizara ya Mambo ya nje ya mamlaka ya Palestina na kundi la Hamas wamelaani shambulio hilo, na kusema Israel ilikuwa inaangamiza mfumo wa afya wa Gaza. Mashambulizi hayo yanafanyika wakati ambapo viongozi wa Hamas wapo mjini Cairo kwa mazungumzo na wapatanishi wa Misri juu ya njia ya kuunusuru mkataba wa kusitisha mapigano.